Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUKACHAGUE VIONGOZI TUWATAKAO KUEPUSHA LAWAMA NA MALALAMIKO



Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo

Wananchi wa Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wamejitokeza kwa wingi kuhamasisha Watanzania kutumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Wakizungumza na Central News leo Jumatatu, Oktoba 13, 2025, wananchi hao wamesisitiza umuhimu wa kila aliyejiandikisha kwenye daftari la wapigakura kujitokeza na kufanya maamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo katika ngazi zote.

Mkazi wa Mapinga, Fatuma Mkumba, amesema amejipanga kushiriki zoezi hilo akiwa na familia yake, akisisitiza kuwa kutokupiga kura ni sawa na kutoa nafasi kwa kuchaguliwa viongozi wasiowataka.

“Tarehe 29 nitaamka asubuhi na familia yangu yote tutaenda kupiga kura. Nawasihi Watanzania wenzangu tutumie haki yetu ya kikatiba, tujitoe kwa wingi tukapige kura kuwachagua viongozi tunaowataka. Ukikosa kupiga kura, utachaguliwa kiongozi usiyemtaka, na mwisho wake ni malalamiko,” amesema Mkumba.

Wananchi wengine wameeleza kuwa viongozi bora na wenye maono chanya ndio msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu kupima sera, ahadi na mipango ya wagombea kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho.

Kwa upande wake, Bi. Tukae Rashid, mkazi wa Mkoa wa Pwani, amewashauri wapigakura kuheshimu sheria na taratibu za uchaguzi kwa kuondoka vituoni mara baada ya kupiga kura, badala ya kubaki “kulinda kura” kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakihamasisha.

 “Ni muhimu kuonyesha nidhamu wakati wa uchaguzi. Baada ya kupiga kura, turudi nyumbani au kazini, tukiwa na imani kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitafanya kazi yao ipasavyo,” amesema.

Aidha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia Watanzania wote kuwa siku ya upigaji kura itakuwa salama na yenye amani. Amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika zoezi hilo la kidemokrasia bila hofu wala vitisho.

Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa kisiwa cha amani, na amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi, kupiga kura kwa utulivu, na kuepuka kushiriki katika maandamano au vurugu zinazoweza kuhatarisha usalama wa taifa.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com