Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SOVELLA AENDELEA KUTOA AHADI ZA MAENDELEO MTAA KWA MTAA KATA YA MSHANGANO

Mgombea nafasi ya Udiwani kata ya Mshangano Benson Sovella aAkizungumza na wananchi na wanachama waliojitokeza kumsikiliza katika mtaa wa Muhombezi 

Na Regina Ndumbaro Mshangano-Songea 

Mgombea nafasi ya udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Mshangano, Benson Sovella, ameendelea na kampeni zake kwa kutembelea mtaa wa Muhombezi leo tarehe 20 oktoba ambapo amewaomba wananchi kumpa kura ili aweze kuwatumikia kwa uaminifu. 

Sovella amezungumza mbele ya wakazi na wanachama wa CCM wa mtaa huo na kuahidi kuwa chama hicho kimejipanga kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara ya kiwango cha changarawe na madaraja, kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya chama.

Sovella amesema kuwa CCM imedhamiria kuboresha huduma za kijamii kwa kujenga madarasa mapya na kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika mtaa wa Muhombezi. 

Amesisitiza kuwa serikali chini ya CCM itaendelea kutekeleza miradi hiyo kwa kushirikiana na wananchi, na kuwaomba wakazi wajitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba kupiga kura kwa ajili ya maendeleo ya kata hiyo.

Sovella pia amewahakikishia wananchi kuwa uongozi wake utakuwa wa uwazi, unaoshirikisha wananchi katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi. 

Ameeleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni mbili zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Mshangano, hasa katika sekta za elimu, afya na mikopo ya vijana na wanawake. 

Amebainisha kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, CCM imepanga kujenga kituo cha afya cha kisasa chenye ghorofa katika kata hiyo.

Kwa upande wao, wazee wa mtaa wa Muhombezi wameonesha kumuunga mkono Sovella, wakimtaka awe diwani wa kudumu badala ya mabadiliko ya mara kwa mara ya madiwani katika kata hiyo. 

Mzee Ndindi amesema kuwa mabadiliko ya madiwani kila wakati yanarudisha nyuma maendeleo, hivyo wanamwomba Sovella awe kiongozi wa kudumu katika kata yao.

 Mzee Hamisi Mustafa ameeleza kuwa yeye na familia yake wamejipanga kwenda kupiga kura na hawana mpango wa kuiacha CCM kwa sababu chama hicho kimeleta maendeleo kwa vipindi mbalimbali. 

Amesema kuwa maendeleo hayaji mara moja, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na subira na kuendelea kukiamini chama cha Mapinduzi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com