Na mwandishi wetu, Iringa
Mufti wa Tanzania Abubakar Zubeir Ali Mbwawa, amewataka waumini wa dini ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi Jumatano, Oktoba 29, 2025, kushiriki kupiga kura kwa kudumisha amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika mkutano maalum wa viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu uliofanyika Msikiti wa Taqwa, Mwembetongwa, Mjini Makambako mkoani Njombe, Mufti Abubakar alisema amani ni nguzo kuu ya ustawi wa taifa na ni wajibu wa kila Muislamu kuilinda na kuihubiri.
“Niwakumbushe kuwa Mtume wetu ni Mtume wa amani, ni Mtume wa kheri, Mtume wa baraka, na ameitangaza amani kama alivyoitangaza Mungu. Vijana, amani ndiyo jambo kubwa kuliko yote.
Msidanganywe na mtu yeyote anayelenga kuivuruga. Muislamu, kila jambo ukiambiwa, fikiria kama linafaa au halifai. Lindeni amani, chungeni amani, na kila mkipata hadhara, simameni, semeni na hubirini kuhusu amani,”
amesisitiza Mufti Abubakar.
Amesema maendeleo na utulivu wa kisiasa hayawezi kupatikana bila amani, hivyo kila mwananchi ana jukumu la kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kisiwa cha amani na mshikamano.

Social Plugin