Na Mwandishi wetu, DAR
Ushahidi unaonesha wazi kuwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania una tija kubwa kwa maendeleo ya Taifa, licha ya mitazamo inayodai kwamba kushiriki uchaguzi ni kupoteza muda. Kinyume chake, kupiga kura ni heshima, wajibu na silaha ya kidemokrasia inayotambulika duniani kote.
Mchambuzi wa siasa, Ally Said, anafafanua kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba inayompa kila Mtanzania nafasi ya kushiriki katika maamuzi ya nchi kwa njia ya amani.
Kupitia kura, wananchi huamua nani awaongoze katika nafasi za kisiasa kama Rais, Wabunge na Madiwani hivyo kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa Taifa na kuhakikisha sauti ya wananchi inasikika.
“Wananchi wanapojitokeza kwa wingi kupiga kura, wanapata fursa ya kuchagua viongozi waadilifu na wenye maono ya maendeleo. Kura ni chombo cha kuwawajibisha viongozi na kuimarisha misingi ya demokrasia,” amesema Ally Said.
Kwa mujibu wake, kupiga kura ni njia sahihi ya kushughulikia changamoto za huduma duni za jamii, kwani viongozi wanaochaguliwa kwa misingi ya uwajibikaji hujua kuwa wanaweza kuondolewa madarakani endapo hawatatimiza wajibu wao.
John James, mkazi wa Goba jijini Dar es Salaam, anasema anafahamu haki yake ya kupiga kura na anawahimiza Watanzania wenzake kuchagua viongozi wanaojua shida za wananchi.
“Mabadiliko ya kweli hupatikana kupitia kura, si vurugu, matusi au maandamano yasiyo halali,” amesema.
Kupiga kura kunatoa nafasi kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika maamuzi yanayogusa maisha yao ya kila siku. Viongozi wanaochaguliwa kwa ushirikiano wa wananchi huwa na uwezo mkubwa wa kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo inayolenga mahitaji halisi ya maeneo yao.
Wito unatolewa kwa kila mwenye sifa ya kupiga kura kujitokeza kwa amani ifikapo Oktoba 29, 2025, kuheshimu sheria za nchi, na kuepuka vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuvuruga uchaguzi.
Kwa pamoja, Watanzania wanapaswa kutambua kuwa kura ni sauti, nguvu, na wajibu wa kila raia — silaha pekee ya kidemokrasia inayoweza kuleta mabadiliko ya kweli katika Taifa.



Social Plugin