Wimbi la wananchi wa Kata ya Kinyerezi, Jimbo la Segerea, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 16, 2025, limejitokeza kwa wingi katika mkutano wa kampeni ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya UWT Taifa, ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni za CCM Jijini Dar es Salaam, Ndg. Mary Pius Chatanda (MCC).
Katika mkutano huo uliofurika wananchi kutoka mitaa mbalimbali ya Kinyerezi, Chatanda aliwataka Watanzania, hususan wakazi wa Segerea, kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 kupiga kura za NDIYO kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Chatanda pia aliwaomba wananchi hao kumpa kura za ushindi Mgombea Ubunge wa Jimbo la Segerea, Bi. Bonnah Kamoli, pamoja na Madiwani wote wa CCM katika kata zote za Jimbo hilo, akisisitiza kuwa viongozi hao wamekuwa mstari wa mbele kusukuma maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, akinadi Ilani ya CCM 2025–2030, Chatanda alieleza kuwa Dkt. Samia anatosha na anafaa kuendelea kuliongoza Taifa, kwani ametekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM 2020–2025, ikiwemo kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu, na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
“Tanzania ya leo ni ya miradi, ni ya maendeleo, ni ya ufanisi. Dkt. Samia ameifanya nchi yetu kuwa mfano kwa mataifa mengine duniani. Hivyo Oktoba 29 tunatiki NDIYO kwa maendeleo zaidi,” alisema Chatanda huku akishangiliwa na mamia ya wananchi wa Kinyerezi.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionesha hamasa kubwa kwa nyimbo, mabango na fulana za kijani, wakiahidi kutoa ushindi wa kishindo kwa CCM katika ngazi zote za uongozi.



Social Plugin