Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

IGP WAMBURA APIGA KURA, ASEMA HALI NI SHWARI NCHINI



Dar es Salaam, Oktoba 29, 2025

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Camilius Wambura amepiga kura leo Jumatano katika kituo cha kupigia kura cha Mbweni, Jijini Dar es Salaam, huku akiwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya Kikatiba katika Uchaguzi Mkuu unaoendelea kote nchini.

Akizungumza mara baada ya kupiga kura, IGP Wambura amesema hali ya usalama nchini ni shwari na hakuna tishio lolote la uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi la upigaji kura linafanyika kwa utulivu na amani.

“Tunaendelea kufuatilia mwenendo wa uchaguzi katika maeneo yote. Hadi sasa hakuna tukio lolote linaloashiria kuvunjika kwa amani. Tunawahakikishia wananchi wote kuwa wako salama na waendelee kujitokeza kupiga kura kwa utulivu,” amesema IGP Wambura.

Ameongeza kuwa askari polisi wapo katika vituo vyote vya kupigia kura kwa ajili ya kutoa ulinzi, kuhakikisha wananchi wanatekeleza haki yao bila hofu, huku akisisitiza kuwa Jeshi hilo halitavumilia mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.

IGP Wambura amehitimisha kwa kuwasihi wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, akisema amani ni msingi wa maendeleo ya Taifa.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com