Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DAR YAONESHA UTAYARI WA KUPIGA KURA,YAKEMEA WITO WA MAANDAMANO



Na Dotto Kwilasa, Dar

Wananchi Mkoani Dar es Salaam wameeleza utayari wao kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, huku wakijitenga na ushawishi unaoenezwa mitandaoni unaohamasisha maandamano na kutopiga kura.

Wameeleza kuwa wanatambua vyema umuhimu wa kudumisha amani na utulivu wa nchi, wakionya dhidi ya vurugu ambazo mara nyingi husababisha vifo, majeraha na kuporomoka kwa uchumi.

Pantaleo Mushi, mkazi wa Mbezi Beach, amesema anatambua jukumu lake la kikatiba la kupiga kura, akiwahamasisha vijana wengine kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao hiyo.

Amefafanua kuwa kutopiga kura ni sawa na kuruhusu kuchaguliwa kwa kiongozi asiyemtaka, jambo ambalo linaweza kuathiri mustakabali wa taifa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo katika ngazi ya kata, jimbo na hata nafasi ya urais.

Kwa upande wa, Said Nassor na Yusuph Ibengwe wakazi wa Kawe wamesema hawana taarifa yoyote kuhusu maandamano yanayodaiwa kuandaliwa.

Wamewataka wananchi wasikubali kurubuniwa na watu wenye maslahi binafsi wanaotaka kuharibu amani ya Tanzania huku Wakiwahimiza Watanzania wote kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura kwa amani, kuepuka vurugu na kutoshiriki katika vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha usalama siku ya uchaguzi.

Wachambuzi wa masuala ya siasa nao wamesisitiza kuwa mabadiliko halisi huanzia kwenye sanduku la kura kwa kueleza kuwa kupiga kura si haki tu bali ni wajibu wa kila raia.

Kwa mujibu wao, kutokushiriki katika uchaguzi ni sawa na kumpa mtu mwingine mamlaka ya kuamua hatma yako.

Wamewahimiza wananchi kutokupoteza sauti yao, wakikumbusha kuwa kila kura ina thamani kubwa katika kuunda jamii na serikali wanayoitaka kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com