Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AHMED ALLY SALUM AHITIMISHA KAMPENI KWA KISHINDO..."TUNAENDA KUIWEKA SOLWA KWENYE KASI MPYA YA MAENDELEO"

Na Mwandishi wetu - Shinyanga

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ahmed Ally Salum, amehitimisha kampeni zake kwa kishindo katika Kata ya Lyabusalu, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025 na kuwachagua wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.

Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Lyabusalu leo, Ahmed amesema kampeni za CCM zimekuwa za amani, umoja na matumaini, zenye lengo la kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Solwa.

“Nawaomba wananchi wote wa Solwa, Oktoba 29 tujitokeze kwa wingi kupiga kura. Tumpigie kura Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi Ahmed Ally Salum kwa nafasi ya Ubunge, na madiwani wetu wote wa CCM. Tukifanya hivyo tutaiweka Solwa kwenye kasi mpya ya maendeleo,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa amepata mapokezi mazuri katika kata zote alizopita wakati wa kampeni, jambo linaloonyesha imani kubwa ya wananchi kwa CCM na kwa serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Nawashukuru kwa imani na upendo wenu. Mmeonesha kiu ya maendeleo, nami naahidi kuendelea kushirikiana nanyi katika kuboresha huduma za afya, elimu, barabara, kilimo na upatikanaji wa umeme. Nipeni ridhaa tuendelee kufanya kazi,” amesema Ahmed huku akishangiliwa na wananchi.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Ndugu Odilia Ibrahim Batimayo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, amewaomba wananchi wa Lyabusalu na maeneo yote ya Jimbo la Solwa kuhakikisha wanashiriki kwa amani katika uchaguzi na kuichagua CCM kwa maendeleo endelevu.

“Chama Cha Mapinduzi kimeonesha dira sahihi ya maendeleo chini ya Rais Dkt. Samia. Ni wakati wa Solwa kuilinda heshima hiyo kwa kumpa kura Dkt. Samia, Ahmed Ally Salum na madiwani wa CCM. Ushindi wa CCM ni ushindi wa wananchi,” amesema Odilia.

Naye Mgombea Udiwani wa Kata ya Pandagichiza, Philipo Mnengula, amewaomba wananchi kumuamini Ahmed kama kiongozi mwenye nia ya dhati ya kuwatumikia, akisema kazi zake zilizotekelezwa awali ni kielelezo cha uongozi makini na wa mfano.

“Tumeshaona kazi zake – kutoka miradi ya maji, barabara hadi shule. Ni mtu wa matokeo, siyo maneno. Tuendelee kumwamini Ahmed,” amesema Mnengula.

Mkutano huo umehudhuriwa na maelfu ya wananchi waliovalia rangi za kijani na njano za CCM, wakipiga makofi, nyimbo na nderemo, wakiapa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika ngazi zote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com