Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AMANI NDIYO HIFADHI YA MWANADAMU, TUILINDE VIONGOZI WA DINI



Viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini wamekutana leo Jumatano, Oktoba 22, 2025, Mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, kwa ajili ya semina maalum ya kujadili umuhimu wa kulinda amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Katika kikao hicho, viongozi hao wamesisitiza kuwa amani ndiyo hifadhi kuu ya mwanadamu, na kwamba hakuna haki, uhai, wala usalama ikiwa taifa halina amani. Wameeleza kuwa jukumu la kulinda amani si la serikali pekee, bali ni la jamii nzima bila kujali dini, kabila au itikadi za kisiasa.

Akizungumza kwenye semina hiyo, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Shaaban Mlewa, amesema kuwa amani hujengwa kwa jamii inayothamini umoja, utulivu na kuheshimiana, huku akisisitiza kuwa raia mwema ni yule anayechangia kuleta amani kwa wengine.

 “Raia mwema ndiye anayeleta amani kwa wengine. Kuitafsiri amani ni kuepuka kila aina ya maudhi, iwe ya kimwili au ya maneno. Hii inasaidia kujenga imani na utengamano miongoni mwa wananchi wote bila kujali tofauti zao,” amesema Sheikh Mlewa.


Kwa upande wake, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Bin Juma, amesema kuwa amani iliyopo nchini ni hazina kubwa inayopaswa kulindwa na kuhifadhiwa na kila Mtanzania. Amesema kuwa ni wajibu wa kila mmoja kupinga vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani hiyo.

Awali, wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Godfrey Mnzava, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alitoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akiwahakikishia usalama na mazingira tulivu wakati wa kampeni, upigaji kura na hata baada ya uchaguzi kumalizika.

Viongozi hao wa dini wameahidi kuendelea kutumia majukwaa yao kuhimiza upendo, umoja na utulivu, wakisisitiza kuwa kulinda amani ni wajibu wa kila Mtanzania.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com