
Shule ya Sekondari Hope Extended Excellence iliyopo mjini Shinyanga imefanya mahafali yake ya tatu ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2025.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Oktoba 19,2025 ikihudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi na wageni waalikwa mbalimbali,
Mkurugenzi wa shule hiyo, Bi. Bahati Bulongo, alisema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2020 ikiwa na wanafunzi tisa pekee, imepiga hatua kubwa za kimaendeleo hadi kufikia wanafunzi 97 mwaka huu 2025.
Bi. Bulongo amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya uongozi wa shule, walimu na wazazi, sambamba na kujituma kwa wanafunzi katika masomo yao.
“Tunamshukuru Mungu kwa hatua hii. Tumefanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi, kupata walimu mahiri, kufanya vizuri kwenye mitihani ya ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga, pamoja na kujenga mabweni, bwalo la chakula na jiko,” amesema Bi. Bulongo.
Aidha, ameeleza kuwa shule imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma ambapo mwaka 2023 wanafunzi wa kidato cha nne walifaulu kwa kiwango cha juu, huku mwaka 2024 wanafunzi wake wakishika nafasi ya pili kimkoa na tatu kimkoa.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa shule pia imeanza kutoa elimu ya stadi za kazi na amali kama vile kilimo, upishi na ufugaji, ili kuwaandaa wanafunzi kujitegemea baada ya masomo.
Pamoja na mafanikio hayo, Bi. Bulongo ametaja changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa kuwa ni ukosefu wa uzio katika eneo la shule, jambo linalohatarisha usalama.
“Tunawaomba wadau, wazazi na wageni waalikwa tushirikiane katika kufanikisha ujenzi wa uzio wa kudumu kwa ajili ya usalama wa watoto wetu,” amesema.
Kuhusu mikakati ya baadaye, uongozi wa shule umedhamiria kuanzisha Chuo cha VETA, Academy ya michezo, na kisima cha maji cha kudumu ili kuboresha zaidi mazingira ya kujifunzia.
Bi. Bulongo amewashukuru wazazi na wageni wote waliohudhuria mahafali hayo kwa ushirikiano wao, akiahidi kuendelea kushirikiana nao kuinua kiwango cha elimu na nidhamu kwa wanafunzi.
“Tuna imani kuwa kwa ushirikiano huu, Hope Extended itaendelea kuwa taa ya maarifa, maadili na ubunifu mkoani Shinyanga,” amesema kwa matumaini.

















































Social Plugin