Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Mhe.Peter Masindi akizungumza kwenye sherehe za kilele cha wiki ya simba ngazi ya Wilaya Septemba 10,2025 katika uwanja wa ukumbi wa Wande Pub Wilayani humo
Na Sumai Salum – Kishapu
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Mhe. Peter Masindi, amewataka vijana kuiona michezo kama fursa ya kujiongezea kipato, kujenga mshikamano na kupanua mtandao wa marafiki badala ya kuichukulia kama burudani pekee.
Mhe. Masindi ameyasema hayo leo Septemba 10, 2025, alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kilele cha Simba Day huku Wilaya ya Kishapu zikiambatana na matukio na michezo mbalimbali na kufuatilia tukio kubwa la kitaifa linalofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Amesema klabu ya Simba sio tu inaiwakilisha Tanzania kimataifa kupitia michezo ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa, bali pia imekuwa ni kivutio kikubwa cha mapato, heshima na kutangaza utalii wa nchi.
“Simba ni timu inayotupa heshima kitaifa na kimataifa. Vijana wanapaswa kuiga nidhamu, mshikamano na bidii inayowaongoza wachezaji hawa kufanikisha ndoto zao,” amesema Mhe. Masindi.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuenzi amani kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio la siku moja tu, huku maisha na maendeleo yakiendelea baada yake.
“Uchaguzi ni siku moja, kisha maisha mengine yanaendelea. Msikubali kushawishiwa kuvunja amani. Wasikilizeni wagombea kwa sera, msiwatusi Wala kuwakejeli. Kisha ifikapo siku ya kupiga kura, chagueni mnapoona atawaletea maendeleo ,msigombane Wala kuwa na chuki isiyokoma na wagombea wawe tayari kupokea matokeo kila Moja Mungu atampa sawasawa na alivyomkusudia” ameongeza.
Sherehe hizo za Simba Day zimepambwa na michezo ya mpira wa miguu, burudani, ushiriki wa wadau mbalimbali wa michezo na wananchi wa Kishapu walioungana kwa pamoja kusherehekea tukio hilo Kwa kuwatembelea wagonjwa, ambalo limekuwa likileta mshikamano wa kijamii na hamasa ya michezo kila mwaka.
Social Plugin