Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAIDI YA WANAFUNZI 41,000 SHINYANGA KUANZA MTIHANI WA DARASA LA SABA KESHO

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

JUMLA ya wanafunzi 41,463 mkoani Shinyanga wanatarajiwa kufanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu elimu ya msingi (darasa la saba) kuanzia kesho na keshokutwa, Septemba 10 na 11, 2025.


Katibu Tawala Msaidizi Elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Mkoa huo, Mwalimu Samson Hango, amebainisha hayo leo Septemba 9,2025 wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo.

Amesema kati ya wanafunzi hao, wasichana ni 23,938 na wavulana 17,525. Aidha, wanafunzi wenye mahitaji maalumu ni 54, wakiwamo wasichana 28 na wavulana 26, ambapo 52 wana uoni hafifu na wawili hawana uoni kabisa.

“Mkoa wa Shinyanga tuna jumla ya wanafunzi 41,463 ambao watafanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kuanzia kesho na kesho kutwa,” amesema Hango.

Ametoa wito pia kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwarubuni watoto ili wasifanye vizuri mitihani hiyo kwa malengo binafsi kama kuwaozesha mapema, badala yake wawaunge mkono ili waweze kufaulu na kutimiza ndoto zao.

Vilevile, amesema maandalizi yote yamekamilika ikiwamo kudhibiti tatizo la uvujaji wa mitihani, na kufafanua kuwa wasimamizi wamepewa maelekezo ya kuzingatia maadili, uzalendo na kupewa mbinu za kudhibiti vitendo vya udanganyifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com