Na Regina Ndumbaro-Mtwara
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka Kata ya Likombe, Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, wameandamana hadi ofisi kuu ya chama hicho mkoani Mtwara kupinga uamuzi wa kumwondoa mgombea wao waliyemchagua kupitia kura za maoni.
Maandamano hayo yamefanyika leo, Agosti 14, 2025, saa chache baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uteuzi wa mgombea wa nafasi ya udiwani.
Wakizungumza na waandishi wa habari, wanachama hao wamesema wamepigwa na butwaa na hatua ya kukatwa kwa mgombea Said Salumu Seif, ambaye aliibuka mshindi katika kura za maoni zilizofanyika Agosti 4 mwaka huu.
Katika kura hizo, Said alipata kura 172, akifuatiwa na Mwinyi Mzaina aliyepata kura 133, huku Husna Mnandoa akiambulia kura 13 pekee.
Wanachama hao wamesema hawajaridhishwa na mabadiliko ya ghafla yaliyoonekana kupuuza maamuzi ya wanachama wa ngazi ya msingi.
Viongozi wa CCM mkoa wa Mtwara wamewasiliana na baadhi ya wanachama waliokuwa wakiandamana na kuwaelekeza kurudi katika ofisi hizo kesho, Agosti 15, kwa ajili ya mazungumzo zaidi.
Hata hivyo, hatua hiyo haikuweza kuondoa hasira na masikitiko ya wanachama walioonekana kutoridhika na majibu yaliyotolewa na viongozi wa chama katika ngazi ya mkoa.
Wanachama hao wamesisitiza kuwa wanachotaka ni haki itendeke na mshindi wa kura za maoni apewe nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Wameonya kuwa ikiwa sauti yao haitasikilizwa, chama hicho huenda kikakumbwa na mtikisiko wa kisiasa katika kata hiyo kutokana na kupoteza uungwaji mkono wa wanachama wa mashinan
Wanachama wa chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Mtwara wakiwa katika ofisi kuu ya chama hicho Wakilalamikia Matokeo ya Udiwani Likombe

Social Plugin