Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SACP Dkt. DEBORA MAGILIGIMBA AONGEZEWA MAJUKUMU SHIRIKISHO LA POLISI WANAWAKE DUNIANI - IAWP


Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Dkt. Debora Magiligimba, ambaye ni Mratibu wa Shirikisho la Polisi Wanawake Duniani (International Association of Women Police – IAWP) kwa Ukanda wa 21 unaojumuisha nchi za Kusini mwa Afrika, ameongezewa majukumu mapya ya kuratibu pia shughuli za IAWP kwa Ukanda wa 20 unaohusisha nchi za Afrika Mashariki.

Awali, Dkt. Magiligimba alikuwa Mratibu wa Ukanda wa 21 (Region 21 Coordinator) unaojumuisha nchi 11. Kwa uteuzi huu mpya, atakuwa mratibu wa jumla ya nchi 25 zilizoko barani Afrika, kufuatia kuunganishwa kwa Ukanda wa 20 (nchi 14) na Ukanda wa 21 (nchi 11).

Nchi atakazoratibu ni: Ukanda wa 20 – Afrika Mashariki (nchi 14): Burundi, Comoros, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mayotte, Reunion Island, Rwanda, Seychelles, Somalia, South Sudan, Uganda pamoja na Ukanda wa 21 – Kusini mwa Afrika (nchi 11): Angola, Botswana, Lesotho, Malawi, Mozambique, Namibia, South Africa, Swaziland, Tanzania, Zambia, Zimbabwe.

Mbali na majukumu hayo, Dkt. Magiligimba pia ni Mjumbe wa Kamati ya Fedha ya IAWP, nafasi inayomuwezesha kushiriki katika maamuzi ya kimkakati ya shirikisho hilo katika ngazi ya kimataifa.

Uteuzi huu, uliofanywa na Rais wa IAWP, Bi Julia Jaeger wa Uingereza, ni heshima kubwa kwa Dkt. Magiligimba na ishara ya imani kubwa kwa uwezo wake wa kiutendaji, uongozi, na mchango wake katika kuendeleza haki, usawa wa kijinsia, pamoja na kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Kupitia nafasi hii, ataendelea kuiwakilisha vyema Tanzania na bara la Afrika katika juhudi za kuimarisha uwezo wa polisi wanawake na wanawake wengine wanaofanya kazi katika vyombo vya utekelezaji wa sheria duniani.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com