Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali ya Tanzania imeanza rasmi safari ya kuibadilisha Dodoma kuwa miongoni mwa vituo vikuu vya utalii barani Afrika, kupitia uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kuendeleza Utalii wa Mkoa huo, ambao sasa unalenga utekelezaji wa vitendo unaoambatana na uwekezaji, uratibu na ushirikishwaji wa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo, amesema muda wa maandiko ya mipango umekwisha, na sasa ni wakati wa kuchukua hatua thabiti zinazolenga kuiweka Dodoma kwenye ramani ya dunia ya utalii.
“Mkakati huu si tu waraka wa maono, bali ni chombo cha mageuzi kwa mkoa huu,” alisema, akiweka bayana kuwa Dodoma ina fursa halisi na za kipekee ambazo hazijatumika ipasavyo katika kukuza utalii na uchumi wa ndani.
Katika kuelezea vivutio vya kipekee vya Dodoma, Mhe. Jafo alitaja mvinyo wa asili, historia ya wapigania uhuru, maeneo ya urithi wa taifa, pamoja na kuanzishwa kwa kijiji cha utalii wa Wagogo kitakachohifadhi na kuonyesha nyimbo, mapishi, mavazi na maisha ya jadi.
Alibainisha pia kuwa miradi mikubwa ya miundombinu kama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato na reli ya kisasa (SGR) inapaswa kuandaliwa kimkakati kwa kuambatana na huduma za utalii ili kuufungua mkoa huo kwa wageni kutoka mataifa mbalimbali.
“Utalii unaanza na wewe,” aliongeza, akisisitiza kuwa kila mwananchi anayo nafasi ya kuwa balozi wa vivutio vya eneo lake.
Pia amesisitiza kuwa hazina ya mila, lugha, mavazi na mapishi ya Wagogo, Warangi, Wasandawe na Waburunge inaweza kutumika kama bidhaa ya kiutalii na urithi wa taifa.
Amesisitiza kuwa Serikali mafanikio ya mpango huu yatatokana na mshikamano wa wadau wote ikiwemo sekta binafsi, vijana, viongozi wa kijamii na wawekezaji.
Amesema serikaki pia Imedhamiria kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji, kurahisisha vibali na kujenga miundombinu bora itakayowezesha utalii kustawi kwa kasi na kwa tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, alisema mkakati huo umejengwa juu ya msingi wa kaulimbiu ya “Ipeleke Dodoma Kimataifa, Ilete Dunia Dodoma,” ambayo sasa imepewa sura ya utekelezaji.
Akitaja maeneo ya misitu ya hifadhi ya Swagaswaga na Mkungunero, historia ya Kongwa kama makazi ya wapigania uhuru, pamoja na majengo ya kihistoria kama Bunge la Jamhuri na Ikulu ya zamani, Senyamule alisema mkoa huo una uwezo mkubwa wa kutoa utalii wa kipekee wenye mvuto wa kimataifa.




Social Plugin