Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Katika sura mpya ya kuibadilisha Dodoma kuwa kitovu cha utalii wa ndani na kimataifa,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameshuhudia ndoto yake ikitima kwa kushuhudia uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kuendeleza Utalii huku akibainisha vyanzo mbalimbali vya kipekee vinavyoweza kuubadilisha mkoa huo kuwa
Akiwa mstari wa mbele katika mapinduzi haya, Senyamule amesisitiza kuwa huu si wakati wa kutazama nyuma, bali kuchukua hatua madhubuti za kuipeleka Dodoma kimataifa kwa vitendo.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo leo Agosti 12,2025 Jijini hapa amesema, "Hatutaki Dodoma ibaki kuwa tu makao ya kisiasa tunataka iwe dira ya kiutalii kwa taifa na nje ya mipaka," amesisitiza kwa msukumo mkubwa.
Kwa kuzingatia kaulimbiu ya Ipeleke Dodoma Kimataifa, Ilete Dunia Dodoma "
"Take Dodoma to the World, Bring the World to Dodoma"Senyamule ameweka bayana kuwa utalii wa asili na wa kiutamaduni ni silaha ya mkoa katika kuvutia wageni na kuimarisha uchumi wa ndani.
Ametaja tamaduni za Wagogo, Warangi na Wasandawe kama hazina huku akieleza kuwa ngoma, mavazi, mapishi ya kienyeji, na lugha asilia ni bidhaa za kiutalii zenye mvuto mkubwa kimataifa.
Mkuu huyo wa mkoa pia hakusita kuangazia vivutio vya kiasili kama misitu ya hifadhi ya Swagaswaga na Mkungunero, pamoja na utalii wa kilimo kupitia mashamba ya zabibu .
Ameeleza kuwa maeneo haya yana uwezo mkubwa wa kuwavutia watalii wanaopenda mazingira halisi ya Kiafrika, wapenzi wa kupiga picha kwenye mandhari zinazovutia na hata wawekezaji katika sekta ya kilimo hai.
Vilevile, ameelezea umuhimu wa kutumia majengo ya Mji wa Serikali,SGR,Bunge, Mahakama Kuu,Bwawa la Mtera na Ikulu kama vivutio vya ziara rasmi na kitaaluma, huku akiweka mkazo juu ya historia ya Kongwa kama urithi wa wapigania uhuru wa Afrika.
Kwa ujumla, amewataka wadau wote wa sekta binafsi, jamii, vijana na wawekezaji kushirikiana nae katika kuiunda upya Dodoma kama mji wa urithi, fursa, na utalii endelevu.
Alieleza kuwa mapishi ya kienyeji, ngoma, lugha na mavazi ya asili ni bidhaa za kiutalii zinazoweza kuuzwa kwa dunia nzima kupitia maonyesho, makumbusho na matamasha ya kimataifa.
"Kwa sasa, mashamba na viwanda vya zabibu vinaweza kutumika kama njia ya kuileta dunia Dodoma kwa kupitia watalii wa kilimo, wahamasishaji wa afya, na wawekezaji wanaovutiwa na uzalishaji wa bidhaa asilia," amesema
Kwa upande wa historia, Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa maeneo kama Kongwa ambayo yalikuwa makazi ya wapigania uhuru kutoka mataifa ya Afrika ni dhahabu ya kihistoria inayopaswa kung’arishwa kwa hadhira ya kimataifa.
“Hatuwezi kuipeleka Dodoma kimataifa bila kuiweka historia yetu katika ramani ya dunia,natoa wito kwa sekta binafsi, jamii za wenyeji, vijana na wawekezaji kuungana na Serikali katika kuiunda Dodoma mpya mji wa urithi, fursa na utalii endelevu, "amesema.








Social Plugin