Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MGOMBEA URAIS DP ACHUKUA FOMU, AAHIDI MAGEUZI YA MAISHA YA ASKARI MAGEREZA, WASTAAFU


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mgombea urais wa Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya, leo Agosti 13, 2025, amekuwa wa 12 kuchukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, akiambatana na mgombea mwenza wake, Sadous Abrahaman Khatib.

Akiwasilisha vipaumbele vyake, Mluya ameanza kwa kuahidi marekebisho makubwa ya mfumo wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu, akieleza kuwa mfumo wa sasa umekuwa chanzo cha dhuluma na kero kubwa kwa watumishi waliolitumikia taifa kwa uaminifu.

Amesema kikokotoo kipya kitazingatia haki ya mfanyakazi kupata stahiki zake kwa kiwango kamili bila kupunguzwa, na kitakuwa chombo cha kuondoa umaskini, kujenga misingi imara ya ajira bora, na kuhakikisha kila mwajiriwa anastaafu kwa heshima na ustawi wa kifamilia.

Pia ameahidi kuwa marekebisho hayo yataenda sambamba na mipango ya waajiri kuwapatia wafanyakazi nyumba bora, hatua itakayopunguza rushwa na kuongeza ari ya kazi.

Ametoa msisitizo kwa Kipaumbele kingine cha mageuzi katika Jeshi la Magereza, ambapo ameeleza dhamira ya kurejesha ubora wa maisha ya askari ili kuwatofautisha na wafungwa.

Mluya amesema hali ya sasa imefikia hatua ambapo askari magereza hawawezi kutofautishwa na wafungwa kutokana na changamoto za mazingira duni ya kazi.

Ameahidi kuboresha mafunzo, maslahi na mazingira ya kazi ili askari waheshimike .

Pia ameahidi kuongeza mishahara ya askari polisi ili kupunguza vitendo vya rushwa na kuimarisha nidhamu ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama.

Akizungumzia ustawi wa Mtoto, Mluya ameahidi kuwa Serikali yake itawajibika kutoa bima ya afya ya bure kwa watoto wachanga kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kuzaliwa ambayo itaambatana na huduma zote za lishe .

Aidha, amesema huduma kwa mama wajawazito zitaimarishwa ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto inalindwa kikamilifu.

Miongoni mwa vipaumbele vingine vilivyotajwa na Mluya ni pamoja na kuondoa ada ya kuhifadhi maiti kwa hoja kuwa walipakodi tayari, kukuza kilimo endelevu kwa kuondoa jembe la mkono, na kuongeza pato la taifa kupitia mageuzi ya sekta ya kilimo.














Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com