Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHANJE SACCOS YATOA MIKOPO YA SHILINGI MILIONI 900 KWA WANACHAMA WAKE

Meneja wa Chama cha akiba na mikopo Mahanje Saccos Kassim Masengo akizungumza akiwa ofisini kwake katika halmashauri ya Madaba 

Na Regina Ndumbaro-

Madaba

Chama cha Akiba na Mikopo cha Mahanje (Mahanje SACCOS), kilichopo Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, kimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 900 kwa wanachama wake katika kipindi cha miaka minne. 

Meneja wa chama hicho, Kassim Masengo, amesema mikopo hiyo imetumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo biashara ndogondogo, ujenzi wa nyumba bora, pamoja na kilimo – hasa cha zao la mahindi ambalo ni msingi wa uchumi kwa wakazi wa Madaba na mkoa mzima wa Ruvuma.Masengo amebainisha kuwa chama hicho chenye wanachama 1,733, kimeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa maeneo ya Mahanje, Lituta na Mkongotema kwa kutoa huduma za kifedha, ushauri wa kilimo kupitia mtaalam aliyeajiriwa na chama, pamoja na elimu juu ya matumizi bora ya mikopo. 

Aidha amesema  kupitia mikopo hiyo, wanachama wameweza kuongeza uzalishaji na kuuza zaidi ya tani 90 za mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kipindi cha miaka minne iliyopita.Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Madaba, Sadam Fupi, amesema halmashauri imeendelea kushirikiana kwa karibu na vyama vya ushirika kuhakikisha vinazingatia sheria na miongozo ya Serikali. 

Amesisitiza kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta tija kubwa kwa wakulima, kwa kuwawezesha kuuza mazao yao kwa bei nzuri kupitia minada rasmi, tofauti na miaka ya nyuma ambapo walikuwa wakilazimika kuuza kwa walanguzi kwa bei duni.

Baadhi ya wanachama wa Mahanje SACCOS wamekishukuru chama hicho kwa kuwawezesha kudhibiti matumizi yao ya fedha na kupata huduma za mikopo kwa masharti nafuu. 

Mwanachama Winfrid Mfikwa ameeleza kuwa tangu ajiunge na chama hicho amefaidika kwa kiasi kikubwa, huku mkulima Hamis Malua kutoka kijiji cha Madaba akieleza kuwa ruzuku ya pembejeo kutoka Serikali imesaidia kuongeza tija mashambani. 

Wote kwa pamoja wameitaka jamii ya wakulima kujiunga na SACCOS ili kunufaika na fursa zilizopo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.Baadhi ya wanachama wa Mahanje Saccos Halmashauri ya Madaba wakipata huduma mbalimbali za mikopo 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com