Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Benki ya Ushirika (Coop Bank) kwa kushirikiana na Mfuko wa Pembejeo wa Kilimo (AGITIF) imetangaza mpango wa mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.5 kwa wakulima vijana na wanachama wa vyama vya ushirika nchini.
Hatua hii inalenga kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya kilimo, ikiwemo kuwainua kiuchumi wakulima wadogo vijijini.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Bw. Godfrey Ng’urah, alisema mikopo hiyo itatolewa kupitia vyama vya ushirika ili kuhakikisha inawanufaisha wakulima wengi, hususan vijana na wanawake.
“Benki ya Ushirika kwa kushirikiana na AGITIF tumedhamiria kuchochea kilimo chenye tija kupitia mikopo nafuu. Leo tumetoa Shilingi Bilioni 8.5 kwa wakulima kama sehemu ya juhudi hizo,” alisema Bw. Ng’urah.
AGITIF, ulioanzishwa mwaka 1994, umekuwa ukitoa huduma za kifedha kwa watu binafsi, taasisi na makundi maalum ya kilimo, ukiweka kipaumbele kwa vijana chini ya miaka 40 na wanawake.
Hadi sasa, mfuko huo umeshakopesha zaidi ya Shilingi Bilioni 94 zilizowezesha miradi ya umwagiliaji na kuongeza uzalishaji mashambani.
Bw. Ng’urah alibainisha kuwa Coop Bank itahudumu kama wakala wa kusimamia utoaji wa mikopo hiyo, ikiwafikia wakulima mijini na vijijini kupitia mtandao wa vyama vya ushirika na matawi ya benki hiyo nchini kote.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dkt. Hussein Mohamed Omar, aliwasihi wakulima wanaonufaika na mikopo hiyo kuhakikisha wanarejesha kwa wakati ili kusaidia wengine kupata mikopo kwenye mzunguko unaofuata.
Mpango huu unalingana na jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya kilimo kupitia mitaji nafuu, kuongeza kipato cha kaya na kukuza ajira za vijana vijijini.
Maonesho ya Nanenane mwaka 2025 yanafanyika kwa kauli mbiu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025” na yalifunguliwa rasmi tarehe 1 Agosti 2025 na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango. Maonesho hayo yatahitimishwa tarehe 8 Agosti 2025.

Social Plugin