Makamu Mwenyekiti wa MAMCU Bakari Ado akizungumza na wakulima wa mbaazi wakati wa kutaja bei ya mnada wa zao hilo katika kijiji cha Lukuledi wilayani Masasi Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Mnada rasmi wa zao la mbaazi kwa msimu wa mwaka 2025/2026 umezinduliwa katika kijiji cha Lukuledi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Uzinduzi huo umefanyika kwa usimamizi wa Afisa Biashara na Masoko, Bi Neema Mmavele, ambaye ameeleza kuwa jumla ya tani 8,295.197 za mbaazi zinatarajiwa kuuzwa sokoni msimu huu.
Bi Mmavele amesema kuwa ni matarajio yao kuona wanunuzi wa zao hilo wakijitokeza kwa wingi ili kuhakikisha wakulima wanapata soko la uhakika.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (MAMCU), Bakari Ado, amefafanua kuwa mzigo wa mbaazi uliofikishwa mnadani ni tani 8,295, huku baadhi ya shehena (loti) tatu — yaani loti 50, 52 na 58 — zimeshindwa kuingia mnadani.
Ado amebainisha kuwa kulikuwa na jumla ya loti 61 na zote, isipokuwa hizo tatu, hazikufanikiwa
kupata wanunuzi.
Ameongeza kuwa bei ya juu katika mnada huo ilikuwa shilingi 850 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa shilingi 810.
Katika kuhakikisha uadilifu wa vipimo wakati wa uuzaji wa mazao, Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara, Saidi Huruma Seif, amewataka wakulima na wanunuzi kuhakikisha mizani yote inayoenda kupimia mazao imehakikiwa rasmi.
Amesema mizani halali itawekwa stika pamoja na muhuri maalum (seal), na kusisitiza kuwa kama vipengele hivyo havipo, wakulima wasikubali kuuza mazao yao kwa kutumia mizani hiyo.
Hata hivyo, wakulima wa mbaazi waliotoa maoni yao kupitia mwakilishi wao, Issa Issa, wameeleza masikitiko yao juu ya bei mpya ya zao hilo.
Issa amesema kuwa bei ya mwaka huu ya kati ya shilingi 810 hadi 850 ni ndogo mno ikilinganishwa na mwaka uliopita (2024), ambapo waliuza mbaazi kwa bei ya juu kati ya shilingi 1,800 hadi 2,000 kwa kilo.
Amesema kuwa hali hiyo imewakatisha tamaa na kuvuruga matarajio yao ya kupata faida kutokana na kilimo cha mbaazi.
Wakulima wana matumaini kuwa wadau wa sekta ya kilimo wataingilia kati ili kuhakikisha bei za mazao hususani mbaazi zinakuwa na tija kwa mkulima.
Wamesisitiza haja ya kuwepo kwa mikakati ya kudumu ya kuimarisha soko na kudhibiti uporomokaji wa bei, ili kulinda maslahi ya mkulima wa kawaida.
Wakulima waliojitokeza katika zoezi la uzinduzi wa mnada wa mbaazi katika kijiji cha Lukuledi wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara
Social Plugin