
Katika taarifa yake kwa umma, Katambi amemshukuru Mwenyezi Mungu, viongozi wa chama chake, wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Mgombea wa Urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kumwamini na kumteua kugombea nafasi hiyo nyeti.
“Uteuzi huu si wangu peke yangu bali ni wa wana-Shinyanga Mjini wote na chama chetu kwa ujumla. Ninaomba mshikamano wa dhati ili kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa Rais wetu Dkt. Samia, wabunge na madiwani wa CCM kote nchini,” amesema Katambi.
Akitambua changamoto za mchakato wa kura za maoni uliohusisha wagombea mbalimbali, Katambi aliomba radhi kwa yeyote aliyekwazika wakati wa kinyang’anyiro hicho na kusisitiza kuwa sasa ni wakati wa kusahau tofauti na kuunganisha nguvu kwa maslahi ya chama na wananchi.
“Ninaomba msamaha kwa yeyote niliyemkosea kwa kujua au kutokujua. Kwa upande wangu, nimemsamehe kila aliyekuwa na mtazamo tofauti nami. Tunapaswa kuwa timu moja ya ushindi, maana hatuna Shinyanga Mjini nyingine isipokuwa hii,” ameongeza.
Katambi pia amewataka wanachama wa CCM kujiepusha na vitendo vya usaliti, akisema chama kikiwa imara na wamoja hakitakuwa na hofu ya kupoteza ushindi.
“Wagombea wenzangu wameniahidi kuniunga mkono na tumepokea pongezi nyingi. Sasa ni wajibu wetu kuhakikisha kura za Rais, wabunge na madiwani zinapatikana kwa wingi ili kuendeleza historia ya CCM kushinda kwa kishindo,” amesema.
Uteuzi wa Katambi unamrejesha tena kwenye kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya ubunge, nafasi ambayo aliishikilia tangu mwaka 2020 baada ya ushindi wake mkubwa kwa tiketi ya CCM. Hatua hii inaweka mwelekeo mpya wa kisiasa katika jimbo la Shinyanga Mjini, ambalo limekuwa ngome muhimu ya CCM katika Uchaguzi Mkuu.
HUU NDIO UJUMBE WA KATAMBI
Ndugu zangu, Wana-Shinyanga mjini wenzangu na Watanzania Wenzangu ninaomba kwa hatua hii niseme yafuatayo;
1. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hii ya Uteuzi
2. Ninakishukuru sana chama chetu, Chama Cha Mapinduzi kupitia Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, kwa kuendesha mchakato huu kwa uwazi na kwa kuniteua kuwa Mgombea wa CCM kwa Jimbo letu la SHINYANGA MJINI.
3. Ninamshukuru sana DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, Mgombea wa URAIS kwa tiketi ya CCM na DKT. EMMANUEL NCHIMBI, Mgombea Mwenza wa DKT SAMIA SULUHU HASSAN kwa kuniona naweza kukiwakilisha chama chetu kwenye Jimbo letu la SHINYANGA MJINI kwa niaba yenu wote.
4. Ninawashukuru ninyi Baba zangu, Mama zangu, Kaka zangu, Dada zangu, na Wadogo zangu kwa heshima hii kubwa mliyonipa kwa mara nyingine, Mimi kwa niaba ya Wana-CCM wenzangu waliowania nafasi hii ya UBUNGE wa Jimbo la SHINYANGA MJINI. Mwenyezi Mungu Anitumie kutimiza NJOZI, MAONO yenu katika maisha ya Utumishi wangu. Mwenyezi Mungu anifanye kama chombo tu cha kuona mawazo yetu yote yanazingatiwa kwa upendo na uvumilivu mkubwa bila kujali hali ya mtu.
5. Ninawapongeza sana Watiania wenzangu waliowania Jimbo la SHINYANGA MJINI kwa ticket ya CCM. Ninaomba wote kwa pamoja wanisaidie Mimi na Chama Cha Mapinduzi ili kura za Mgombea Wetu wa URAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN apate kura za kutosha ndani ya Jimbo letu la SHINYANGA MJINI na Mbunge Pamoja na MADIWANI wa CCM washinde kwa kishindo kikuu.
6. Ninawaomba kwa unyenyekevu mkubwa tuwe wamoja katika kukipigania chetu. Mnanifahamu kwamba sipendi SHINYANGA MJINI yenye Makundi, Ninaomba tuwe wamoja katika hali zote. Kwenye mchakato huu wa kuwania Ubunge yamkini tumekwaruzana na kukoseana, Mimi ninaomba kama kuna ambaye nimemkwaza au kumkosea kwa njia moja au nyingine, kwa kujua au kutokujua, ninaomba mnisamehe na Mimi nimemsanehe yeyote aliyekuwa na mawazo tofauti na Mimi na timu yangu ya Kampeni. Kwa sasa ninaomba sana sisi wote tuwe timu moja katika kukitafutia chama chetu ushindi ifikapo Oktoba Mwaka huu.
7. Niwashukuru Wagombea wenzangu kwani mara baada ya Matangazo ya Uteuzi wa Wagombea wa CCM Majimbo ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, Wawakilishi na Wabunge wa Viti Maalum, Wamenipigia Simu na Kunipongeza na pia kuniahidi kuniunga mkono na kukipigania Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu.
8. Ninawaomba Wana-Shinyanga mjini wenzangu ambao ni Wana-CCM tujihadhari sana na usaliti wa aina yeyote kwenye uchaguzi huu kwenye kata zetu, na Jimbo letu. CCM tukiwa wamoja, tutashinda kwa kishindo bila wasiwasi wowote.
9. CCM yetu ipo Imara sana na tusiogope, TUTASHINDA KWA PAMOJA.
10. Ninaomba kuwataarifu kwamba Viongozi wa Chama Chetu wakiweka utaratibu wa kuchukua fomu za Kugombea kwenye Tume ya Uchaguzi, nipo tayari na niwaombe wote kwa pamoja tujumuike kwenye tukio hili la muhimu sana kwenye mchakato wote wa ushindi wa CCM.
11. Ninaomba sana kila mmoja wenu atuombee katika safari hii ya Uongozi wa Jimbo letu kwa nafasi ya Ubunge.
12. Ninawashukuru sana kwa Pongezi zenu wote bila kuwataja majina mmoja mmoja. Asanteni sana. Huu ni ushindi si wangu tu bali ni wetu sote.
13. Ninawapenda sana, “tukutane site” na Mapenzi ya Mungu Yakatimie. Amen.
Social Plugin