Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAWA YAONESHA VIVUTIO VYA UTALII KATIKA MAONESHO YA 49 YA BIASHARA YA KIMATAIFA



Dar es Salaam


Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) inashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, barabara ya Kilwa, Jijini Dar es Salaam.

Kupitia ushiriki wake katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, TAWA inalenga kuhamasisha na kutoa elimu kwa umma kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka hiyo, huku ikitangaza vivutio na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii na uhifadhi wa wanyamapori nchini.

🔹 Fursa za Uwekezaji

Wadau na wananchi wanapata nafasi ya kupewa taarifa za kina kuhusu maeneo yenye fursa za uwekezaji chini ya usimamizi wa TAWA. Maeneo hayo ni pamoja na Makuyuni Wildlife Park (Arusha), Pande (Dar es Salaam), Wami-Mbiki (Morogoro na Pwani), Tabora Zoo (Tabora), Ruhila Zoo (Ruvuma), na mengineyo.

🔹 Wanyamapori Hai

Ndani ya banda hilo, TAWA imeandaa bustani maalum ya wanyamapori hai, ambapo wageni wanapata fursa ya kipekee kuwaona kwa ukaribu wanyama mbalimbali kwa viingilio vya bei nafuu, hasa kwa Watanzania.

🔹 Vivutio vya Utalii

Wananchi pia wanapewa maelezo kuhusu vivutio vilivyopo kwenye maeneo yanayosimamiwa na TAWA pamoja na gharama na taratibu za kuyatembelea, kwa lengo la kuongeza mwamko wa utalii wa ndani.

🔹 OFA Maalum ya Ziara

Katika msimu huu wa maonesho, TAWA imetoa OFA maalum kwa ziara ya kutembelea Hifadhi ya Pande, iliyopo Jijini Dar es Salaam, kwa gharama nafuu zaidi ili kuruhusu wananchi wengi kujionea vivutio vilivyopo.

🔹 Elimu kwa Umma

Maofisa wa TAWA wapo tayari kutoa elimu juu ya namna bora ya kushughulika na wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na kueleza tabia za wanyama hao kwa lengo la kujenga uelewa na kuimarisha uhifadhi.

🔹 Nyamapori Choma

Kwa wapenzi wa vyakula vya asili, TAWA imeandaa huduma ya Nyamapori Choma kwa viwango vya hali ya juu, vyenye ladha ya kipekee na kwa bei ya kizalendo.

Wananchi wote wanakaribishwa kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii kujifunza, kufurahia na kupata uzoefu wa kipekee kuhusu huduma na vivutio vya kiutalii vinavyopatikana nchini kupitia TAWA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com