Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANGA YAJIIMARISHA KUWA KITUO KIKUU CHA UTALII NA BIASHARA KANDA YA KASKAZINI



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkoa wa Tanga umeendelea kujijenga kuwa kitovu cha utalii na uchumi endelevu kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kibiashara, michezo, usafirishaji na urithi wa kihistoria. Kupitia jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanga imepata sura mpya inayovutia wawekezaji, watalii na wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Salha Burian, ameeleza hayo July 15,2025 Jijini Dodoma kwenye mkutano wake na Waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita ambapo ameeleza kuwa maendeleo ya miundombinu ya kibiashara na usafirishaji siyo tu yanalenga kukuza uchumi, bali pia yanauweka Mkoa wa Tanga kwenye nafasi ya kipekee ya kuwa lango kuu la utalii wa Kaskazini-Mashariki mwa Tanzania.

Amesema Kupitia miradi kama ujenzi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Business Centre, soko la kisasa la machinga, pamoja na kituo cha michezo cha TFF kilichopo Mnyanjani, Tanga inazidi kuwa kivutio si kwa watalii wa asili pekee, bali pia kwa watalii wa biashara na michezo.

Aidha,ameeleza kuwa Mkoa umepewa hadhi ya kipekee kwa kuwa mwenyeji wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga, jambo ambalo limefungua milango ya wageni, wataalamu wa kimataifa na wawekezaji wanaofuatilia maendeleo ya kanda hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga amesema mradi huo umezalisha ajira zaidi ya 800 kwenye eneo la Chongoleani pekee, huku shughuli za kijamii na huduma za chakula, usafiri, malazi na burudani zikiimarika kwa kasi. Mwitikio huu umeufanya Mkoa wa Tanga kuwa eneo linalovutia kwa utalii wa uwekezaji (investment tourism).

Katika kuimarisha nafasi ya Tanga katika utalii wa usafiri wa majini amesema, Serikali imefanya ukarabati mkubwa wa kivuko cha MV Tanga kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.1, hatua inayolenga kuwezesha watalii na wananchi kusafiri kwa urahisi kati ya maeneo ya mwambao na visiwa vidogo vilivyopo ukanda huo.

Kwa upande mwingine, maboresho ya Bandari ya Tanga kupitia uwekezaji wa shilingi bilioni 429.1 yameiweka bandari hiyo katika ramani ya kimataifa. Kwa sasa bandari hiyo inahudumia meli zaidi ya 300 kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka meli 198 mwaka 2021.

Aneeleza kuwa Ufanisi huo umefungua milango kwa watalii wanaotumia njia ya majini, hususan kutoka Kenya, Zanzibar, Pemba na maeneo ya Asia Mashariki.

Licha ya hayo ameeleza kuwa Mkoa pia umejipambanua kwa kuwa na vivutio vya kipekee vya utalii wa utamaduni na historia kama vile mapango ya Amboni, mlima Usambara, mji wa kale wa Pangani, pamoja na maeneo ya asili yenye mandhari ya kuvutia pamoja na Uboreshaji wa miundombinu ya barabara na usafiri wa anga katika kanda hiyo unaendelea kufungua zaidi njia kwa watalii wa ndani na wa kimataifa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeonyesha kwa vitendo dhamira ya kuendeleza sekta ya utalii kama injini ya uchumi huku akiwataka wananchi wa Tanga kushiriki kikamilifu katika fursa zinazozalishwa kupitia sekta hiyo, zikiwemo ujasiriamali, huduma za malazi, miongozo ya watalii, bidhaa za asili na maonesho ya utamaduni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com