Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAJENGA BWALO LA CHAKULA MASONYA, YAWAONDOLEA WANAFUNZI KULA CHINI YA MITI

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Denis Masanja akiimba nyimbo pamoja na wanafunzi ya shule ya Wasichana Masonya baada ya kufanya ziara ya kutembelea shuleni hapo 

Na Regina Ndumbaro-Tunduru 

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Masonya iliyopo Wilaya ya Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, wameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuanza ujenzi wa bwalo la chakula litakalowaondolea adha ya kula chini ya miti au madarasani. 

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi Marian Michael amesema bwalo hilo litakuwa msaada mkubwa hasa kutokana na ongezeko la wanafunzi wa kidato cha tano kwa mwaka wa masomo 2025/2026, hivyo ameomba Serikali ikamilishe haraka mradi huo.

Mkuu wa shule hiyo, Makrina Ngonyani amesema kuwa  ujenzi wa bweni hilo ulianza mwezi Juni kwa kusafisha eneo na tayari kazi ya kujaza kifusi katika msingi imekamilika kabla ya kumwaga zege. 

Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi milioni 168, ambapo hadi sasa Shilingi milioni 102.7 zimetumika na kiasi kilichobaki ni Shilingi milioni 65.2. 

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa ni kuongezeka kwa gharama zisizokadiriwa awali kama usafishaji wa eneo, upatikanaji wa maji na ujenzi kwenye eneo lenye mteremko.

Ngonyani ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu shule hiyo imepata mafanikio makubwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi, ikiwemo mabweni manne, madarasa kumi na matundu ya vyoo 15 kwa gharama ya Shilingi milioni 775, na ujenzi wa bweni moja kupitia mradi wa Sequip kwa gharama ya Shilingi milioni 128.

 Pia wamejenga vyumba vinne vya madarasa na vyoo 15 kwa Shilingi milioni 121, jambo lililobadili sura ya shule hiyo ya zamani na kuifanya kuwa na mwonekano mpya wa kuvutia.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja, amefanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwalo hilo na kuwataka mafundi kuongeza kasi ili likamilike kabla ya mvua za masika. 

Aidha, amewapongeza walimu kwa usimamizi mzuri wa fedha na miradi yote, sambamba na kuwahimiza kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuwa na upendo kwa wanafunzi na kusubiri kwa uvumilivu huku Serikali ikiendelea kuboresha mazingira na maslahi yao ya kazi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com