Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kumekucha! KIKAO CHA KUPITISHA WAGOMBEA UBUNGE CCM KUFANYIKA DODOMA


Dodoma, Julai 15, 2025 – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kuwa Kikao cha Kawaida cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kitafanyika tarehe 19 Julai 2025, kuanzia saa nne asubuhi katika Jiji la Dodoma, chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Gabriel Makalla, kikao hicho kitakuwa ni sehemu muhimu ya mchakato wa maandalizi ya uchaguzi, ambapo ajenda kuu ni kupitia na kujadili masuala mbalimbali ya chama na nchi kwa ujumla.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kikao hicho cha Kamati Kuu kitatanguliwa na kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, kinachoendelea jijini Dodoma kwa ajili ya kupokea na kuchambua majina ya wagombea ubunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na uteuzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa Majimbo na Viti Maalum.

Katika kikao hicho, Chama kimeeleza kuwa kitazingatia maadili, sifa na vigezo vya wagombea kabla ya kuwasilisha majina hayo mbele ya Kamati Kuu kwa ajili ya kufanya maamuzi.

Taarifa hiyo ya Chama Cha Mapinduzi imesisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchakato wa kidemokrasia ndani ya chama na maandalizi ya kuelekea uchaguzi mkuu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com