Na Dotto Kwilasa , Dodoma
Katika tukio la kihistoria la uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, mfanyabiashara mashuhuri nchini na mwakilishi wa sekta binafsi, Rostam Azizi, amewasilisha salamu zenye uzito wa kiuchumi na kiutawala, akiipongeza Serikali kwa hatua hiyo ya kimkakati huku akitoa mapendekezo ya msingi kuhusu utekelezaji wa dira hiyo.
Rostam ameanza kwa kusisitiza kuwa msingi wa maendeleo ya taifa lolote hujengwa kwenye kupanga kwa weledi, na kueleza kuwa dira hii inawakilisha maono ya pamoja kuhusu Tanzania ya baadaye.
“Kila hatua ya maendeleo huanzia kwenye kupanga,na ni lazima tukubaliane, sisi Watanzania tunatazama zaidi namna mpango huu unavyotekelezwa kwa ufanisi,” alieleza kwa msisitizo.
Akiwasilisha maoni ya sekta binafsi, Rostam amehimiza uhitaji wa uongozi unaoelekeza ufanisi, huku ukijengwa juu ya misingi ya amani na utulivu, akibainisha kuwa haya ni mambo yasiyopaswa kuchukuliwa kwa wepesi.
“Tunataka uongozi unaoelekeza ufanisi na misingi ya amani na utulivu,tunapowekeza katika rasilimali watu, lazima pia tuhakikishe kuwa tuna uongozi wenye nguvu za kuyabeba na kuyatekeleza matarajio yetu,” amesisitiza.
Katika hoja za kina, amesisitiza umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika rasilimali watu kwa lengo la kuwalea vijana wa Kitanzania katika nyanja mbalimbali za uzalishaji, ubunifu na uongozi.
Amesema dira hiyo inapaswa kuwa chombo cha kulea kizazi kijacho kwa misingi ya maarifa na ustadi.
“Kupitia mpango huu, tutawalea vijana wengi katika nyanja mbalimbali,hii ni fursa ya kihistoria ya kulijenga taifa lenye watu waliokomaa kiujuzi na kifikra,” amesema.
Hata hivyo, Rostam ameonya kuwa mafanikio ya dira hayawezi kupatikana ikiwa sekta binafsi, haswa wafanyabiashara wa ndani, hawatashirikishwa ipasavyo au kuwekewa mazingira rafiki.
Hivyo ametoa wito wa kutungwa kwa sera zinazoinua wafanyabiashara badala ya kuwaumiza, ili kulinda uchumi wa taifa na kukuza ushindani wa ndani.
“Hatutafanikisha haya yote kama tutashindwa kuwajali na kuwatetea wafanyabiashara, Sera zitungwe zinazoweza kuwainua wafanyabiashara na si kuwaumiza ili kulinda uchumi wao,hili ni jambo la msingi,” amefafanua.
Licha ya hayo ameeleza kuwa uwekezaji huu wa kijumla utaleta matokeo chanya katika mapato ya taifa, kwa sababu fedha zitakazopatikana kutokana na ukuaji wa uchumi zitaendeleza maendeleo na si kulipiza visasi, hali itakayojenga mshikamano wa kitaifa na matumaini kwa vizazi vijavyo.
“Tukiweza kuwekeza haya, fedha zitakazopatikana zitaendeleza maendeleo na si visasi,” amesisitiza.
Rostam pia ametumia jukwaa hilo kuipongeza Serikali na Tume ya Mipango kwa kuandaa dira ya muda mrefu yenye mwelekeo wa wazi, akisema kuwa sekta binafsi itaendelea kushirikiana kwa karibu kuhakikisha dira hiyo inatekelezwa kikamilifu kwa manufaa ya wote.
“Sisi sekta binafsi tunaipongeza Serikali na Tume yake ya Mipango,tuendelee kujenga taifa lenye misingi imara ya maendeleo,Sina shaka kwamba Mheshimiwa Rais utatuwekea misingi mizuri na imara itakayowawezesha watakaokuja baadaye kuendeleza dira hii kwa vitendo,” amesema
Pamoja na mambo mengine Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inalenga kulifanya Taifa la Tanzania kuwa la uchumi unaojitegemea, jumuishi, na lenye ushindani wa kimataifa ambapo Sekta binafsi inatajwa kuwa mhimili muhimu wa kufanikisha azma hiyo kupitia uwekezaji, ubunifu na ajira.

Social Plugin