
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizindua Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 mara baada ya uzinduzi katika ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma tarehe 17 Julai, 2025.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 katika hafla ya kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma. Dira hiyo inaweka mwelekeo wa maendeleo ya muda mrefu wa Taifa, ikilenga kuijenga Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa juu, yenye maendeleo jumuishi na endelevu ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Rais Samia ameiagiza Tume ya Taifa ya Mipango kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuandaa mifumo ya kupima utekelezaji wa dira hiyo kwa vitendo, ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya kwa wananchi. Ametoa msisitizo kuwa dira hiyo isiishie kuwa karatasi, bali iwe nyenzo ya kuleta mabadiliko ya kweli.
Dira hiyo imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza, ikihusisha maoni ya makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Inazingatia misingi mikuu mitano: Demokrasia, haki na uhuru; utu, amani na mshikamano; utajiri wa rasilimali asilia; utamaduni na maadili ya taifa; pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo.
Wadau kutoka sekta binafsi wakiongozwa na mfanyabiashara maarufu Rostam Azizi wameipongeza Serikali kwa dira hiyo, wakitoa wito wa utekelezaji wake kwa vitendo, hususan kwa kuwekeza katika rasilimali watu na ubunifu. Dira ya 2050 inatarajiwa kuwa dira shirikishi inayogusa maisha ya kila Mtanzania. Picha : RAIS SAMIA USO KWA USO NA FREEMAN MBOWE UZINDUZI DIRA 2050














Social Plugin