Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AFUNGUA MILANGO YA MATUMAINI: WENYE ULEMAVU WAIPOKEA DIRA YA 2050 KWA MIKONO MIWILI


Mkurugenzi wa FDH akizungumza na Malunde Blog Jijini Dodoma mara baada ya Uzinduzi wa Dira ya 2025.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Mkurugenzi wa Shirika la Foundation for Disabilities and Hope (FDH), Michael Salali, amesema uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ni hatua kubwa ya kihistoria ambayo kwa mara ya kwanza imeweka bayana dhamira ya kujumuisha watu wenye ulemavu katika ajenda kuu za maendeleo ya taifa.

Ametoa kauli hiyo jijini Dodoma mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi dira hiyo leo Julai 17, 2025.

Salali amesema FDH inatambua na kupongeza namna mchakato wa maandalizi ya Dira hiyo ulivyokuwa shirikishi, ukihusisha mawazo ya makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu.

Ameeleza kuwa dira hiyo inakwenda kujibu changamoto nyingi ambazo watu wenye ulemavu wamekuwa wakikumbana nazo kwa miaka mingi, zikiwemo ukosefu wa fursa za kiuchumi, miundombinu isiyo rafiki, upatikanaji hafifu wa elimu jumuishi na huduma duni za afya.

“Kwetu sisi wenye ulemavu, hii dira ina maana kubwa kwa kuwa inaweka mwelekeo wa wazi wa kutatua changamoto zetu kupitia sera na mifumo jumuishi,tunatoa wito kwa watu wote wenye ulemavu kuisoma, kuielewa na kufuatilia utekelezaji wake,” amesema Salali.

Aidha, Salali amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa kuwatambua na kuwawezesha watu wenye ulemavu, akitaja mafanikio kadhaa ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwemo kuimarishwa kwa elimu jumuishi, uwepo wa Sera na Dira mahsusi ya watu wenye ulemavu, ajira serikalini, vifaa saidizi na ushirikishwaji kwenye mabaraza ya maamuzi.

" Haya ni matokeo ya dhamira ya kweli ya Rais kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma katika safari ya maendeleo, "amesema Mkurugenzi huyo wa FDH.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com