Wawakilishi wa Asasi za Kirai wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kufanyika mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro.Mkutano uliandaliwa na NaCongo kwa kushirikiana na serikali ya mkoa wa Morogoro.Picha na Peter Kimath
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mh.Adam Malima akiongea na asasi za kiraia katika Mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro.
**
MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa huo yametekeleza miradi ya maendeleo jumuishi iliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 30 kwa kipindi cha miaka mitano hadi kufikia 2024/2025.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Morogoro, Otanamusu Nicholaus alisema hayo katika mkutano wa tathmini ya mchango wa Mashirika hayo katika maendeleo ya taifa mkoani humo.
Nicholaus alisema mkutano mwaka huu ulibeba mada kuu ni “Tathmini ya mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya Taifa 2020/2021- 2024/25, mafanikio, changamoto,fursa na matarajio”.
Nicholaus alisema fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi ya maendeleo jumuishi, kwa kuzingatia sheria, miongozo na taratibu za nchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo afya hususani kampeni za chanjo.
Pia elimu ya afya ya uzazi na mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, elimu ikiwemo uboreshaji wa madarasa ya awali, mafunzo kwa walimu na uandaaji wa vifaa vya kujifunzia.
Alitaja miradi mingine ni uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti , uhifadhi wa vyanzo vya maji, uwezeshaji wa vijana na wanawake kiuchumi, kupinga ukatili wa kijinsia, utekelezaji wa haki za binadamu, na miradi ya maji safi ikiwemo ya uchimbaji wa visima katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Mwenyekiti wa Mashirika hayo mkoa wa Morogoro alisema katika kipindi cha miaka hii mitano, zaidi ya mashirika 150 yameweza kufanya kazi na kuwasilisha taarifa kwa vipindi tofauti vya kuanzia miezi sita hadi miaka sita ya mikataba ambapo mikataba huombwa upya kila baada ya mwaka.
“Mashirika haya yameendelea kushirikiana kwa karibu na Halmashauri zetu katika kutekeleza mikakati ya maendeleo kwa kushirikisha jamii, huku yakitoa mchango mkubwa katika kuinua maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa mkoa wetu” alisema Nicholaus.
Alisema mafanikio hayo yanadhihirisha kuwa sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali ni mshirika wa kweli wa Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Nicholaus alisema mkoa huo una jumla ya NGOs 571 zilizosajiliwa na kutambuliwa na Serikali, pia mashirika 11 yamesajiliwa kimataifa, 457 kitaifa, 16 kimkoa na 24 katika ngazi ya Wilaya.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huyo Malima,aliwataka wadau wa wote wa mashirika hayo kushiriki kikamilifu katika kuchochea maendeleo ya mkoa huo kiuchumi, kijamii, kielimu na kisiasa badala ya kushiriki kwenye shughuli zinazochochea mgawanyiko na uvunjifu wa amani.
Hivyo aliyatahadharisha mashirika yanayojihusisha na vitendo vinavyohatarisha amani na utulivu ndani ya mkoa huo, hasa kipindi kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na yanayokwenda kinyume na maadili, mila, na desturi za wananchi wa mkoa huo hazitavumiliwa kamwe.
Naye Mkurugenzi wa Agriwezesha, Deogracia Ignas, alisema shirika lake linaendelea kushirikiana na Serikali kwa kugawa miche ya mazao ya mikakati ikiwemo ya parachichi kwa wakulima hatua ambayo inayochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na kuhakikisha amani inaendelea kudumu.
Social Plugin