
Na Woinde Shizza, Arusha
Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika jijini Arusha, Kamishna Badru amesema ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja kati ya wadau mbalimbali wa utalii, wananchi, viongozi, wanafunzi wa vyuo na waandishi wa habari waliobeba ujumbe wa hifadhi hiyo kwa umahiri mkubwa.
“Ngorongoro tunatoa shukrani za dhati kwa kila mmoja aliyechagua kusimama nasi na kupiga kura. Ushindi huu si wa NCAA pekee bali wa Watanzania wote,” alisema Kamishna Badru huku akionesha tuzo mbili za ushindi huo
Kamishna Badru alieleza kuwa Ngorongoro si kivutio cha kitalii tu, bali ni hazina hai ya urithi wa kihistoria, maumbile ya kipekee na utamaduni wa asili.
Alitaja maeneo yenye umuhimu mkubwa kama Nyayo za Laetoli zenye historia ya miaka milioni 3.6, Makumbusho ya Olduvai, Mlima Lomalasin (mlima wa tatu kwa urefu Tanzania) pamoja na uhamaji wa wanyama wa savana unaovutia kila mwaka.
Katika hotuba yake, aliwapongeza pia wageni wa kimataifa waliotembelea eneo hilo, wanafunzi wa vyuo waliounga mkono kampeni ya hifadhi, na waandishi wa habari waliowezesha ujumbe wa Ngorongoro kufika mbali.
Ngorongoro ni moja kati ya maeneo yaliyosajiliwa na UNESCO kama Urithi wa Dunia na Hifadhi ya Hai (Biosphere Reserve), jambo linaloiongezea hadhi ya kipekee katika uso wa dunia.
“Vivutio hivi kwa ujumla vinaiweka Ngorongoro juu na kuwa kivutio bora cha utalii Afrika kwa mwaka 2025,” alihitimisha Kamishna Badru.
Social Plugin