Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika kuhakikisha sekta ya madini inachangia kwa ufanisi ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa, Mkoa wa Mwanza umeanza kuchukua hatua mahsusi kudhibiti na kuratibu shughuli za uchimbaji wa madini kiholela, hususan katika maeneo ya Kasanda na Ishokela Hela, yaliyopo Wilaya ya Misungwi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema kuwa serikali ya mkoa imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, usalama wa wachimbaji unazingatiwa, mazingira yanahifadhiwa na wananchi wananufaika na rasilimali hiyo kwa haki.
“Mwanza ni mkoa unaokuja kwa kasi sana kwenye sekta ya madini. Sasa jukumu la Ofisi ya Afisa Madini Mkazi (RMO) ni kuwafikia wachimbaji, kuwapa elimu, kuwasajili rasmi, na kuhakikisha serikali inapata gawio lake kwa mujibu wa sheria,” amesema Mhe. Mtanda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tayari maeneo mengi yenye shughuli za uchimbaji yamefanyiwa utambuzi rasmi, na wachimbaji wake wanaendelea kupewa elimu ya kitaalam kuhusu taratibu za kisheria, matumizi salama ya vifaa, usimamizi wa mazingira na utunzaji wa mapato.
Mtanda amesema lengo la mkoa ni kuhakikisha wananchi wanaishi na kunufaika na madini kwa vitendo, kwa kuendana na kaulimbiu ya kitaifa inayosema: “Madini ni Utajiri”.
“Tumejipanga kuhakikisha hakuna tena uchimbaji usio rasmi au wenye viashiria vya uharamia. Tunataka sekta hii iwape ajira, iwainue wachimbaji wadogo, na ichangie mapato ya serikali kwa uwazi,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mkoa wa Mwanza unatarajia kupata msukumo mpya wa maendeleo kupitia Mgodi wa Kimataifa wa Nyanzaga, ambao uko katika hatua ya maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza uzalishaji.
Mgodi huo unatarajiwa kuwa moja ya maeneo makubwa ya uwekezaji katika kanda ya ziwa, na utatoa fursa kwa Watanzania hususan wakazi wa Mwanza katika ajira, huduma, biashara ndogondogo na mapato kwa halmashauri husika.
Amesema hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya serikali ya mkoa kuhakikisha kwamba utajiri wa madini unalindwa, unasimamiwa kwa weledi, na kuwanufaisha wananchi badala ya kuwa chanzo cha migogoro au uharibifu wa mazingira.

Social Plugin