Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KASANDA AOKOA MAISHA YA MZEE MASKINI ALIYETELEKEZWA NA FAMILIA YAKE

Gari la wagonjwa likiwa katika eneo la nyumba ya mzee James wakati lilipokuja kumchukua nyumbani kwake kwaajili ya kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi

Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Rachael Kasanda, ameonyesha moyo wa huruma na uwajibikaji kwa vitendo baada ya kumuokoa mzee James, mkazi wa kijiji cha Mpindimbi, aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mguu kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata matibabu yoyote.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 58 alikuwa akiishi katika mazingira magumu baada ya kutelekezwa na familia yake.

Hatua hiyo ilichukuliwa na DC Kasanda mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi walioguswa na hali ya mzee huyo.

Bila kusita, alifika kijijini Mpindimbi na kumchukua mzee James hadi katika hospitali ya wilaya ya Masasi, Mkomaindo, kwa ajili ya matibabu ya haraka.

Kitendo hicho kimepongezwa kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ambao wamesema ni mara ya kwanza kushuhudia uongozi wa aina hiyo wenye kugusa maisha ya watu moja kwa moja.

Mzee James, ambaye kwasasa amelazwa katika hospitali ya Mkomaindo, amesema anashukuru sana kwa msaada aliopata kutoka kwa mkuu huyo wa wilaya.

Ameeleza kuwa amekuwa akiteseka kwa muda mrefu huku akikosa msaada wowote kutoka kwa familia au jamii inayomzunguka.

Hali yake kwa sasa inaendelea kuimarika chini ya uangalizi wa madaktari wa hospitali hiyo.

Serikali ya wilaya ya Masasi kupitia uongozi wa mkuu wa wilaya mheshimiwa Kasanda imesisitiza kuwa itaendelea kuwajali wananchi wote hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu.

DC Kasanda ameahidi kufuatilia maendeleo ya afya ya mzee huyo na kuhakikisha anapona kikamilifu.

Hii ni hatua ya kuigwa na viongozi wengine nchini katika kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma kwenye huduma muhimu kama afya
Mkuu wa wilaya ya Masasi Rachael Kasanda akiwa katika nje ya nyumba ya mzee James katika kijiji cha Mpindimbi wilayani Masasi 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com