Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Tanzania inajiandaa kushuhudia tukio la kihistoria la kuenzi mashujaa wake waliotoa mchango mkubwa kwa uhuru, amani na maendeleo ya taifa, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuongoza maadhimisho hayo Julai 25, 2025, katika Viwanja vya Mnara wa Mashujaa, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Taarifa hiyo imetolewa leo Julai 24, 2025 na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa.
“Huu ni wakati wa kutafakari, kukumbuka na kuthamini sadaka ya mashujaa waliotangulia mbele ya haki. Ni siku ya kutia moyo kizazi cha sasa kuendeleza misingi ya utaifa, mshikamano na uzalendo,” amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali za kiheshima, ikiwemo kuwashwa kwa Mwenge wa Kumbukumbu ya Mashujaa saa 6:00 usiku wa Julai 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa Dkt. Biteko, shughuli za siku ya maadhimisho zitapamba moto Julai 25 kuanzia saa 3:00 asubuhi kwa gwaride rasmi la heshima litakaloongozwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Hitimisho la maadhimisho hayo litaambatana na uzimaji wa Mwenge wa Kumbukumbu saa 6:00 usiku siku hiyo hiyo.
“Tunapaswa kuenzi siku hii kwa kushiriki kwa wingi, kwa sababu inatufundisha thamani ya kujitoa kwa ajili ya nchi yetu. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kuwa shujaa katika nafasi yake,” amesisitiza.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kusaidia kueneza elimu kuhusu umuhimu wa siku hii kwa mustakabali wa Taifa.
“Hii ni siku ya kumbukumbu na kujifunza. Ni wajibu wetu kuwafundisha vijana maana ya ushujaa – siyo tu kushika silaha, bali pia kufanya jambo jema kwa ajili ya jamii na Taifa,” amesema.
Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa hufanyika kila mwaka nchini kote kwa lengo la kuenzi maisha na mchango wa watangulizi waliolinda na kulijenga Taifa. Mwaka huu, maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa ya kipekee kwa heshima ya hali ya juu inayotolewa na Serikali.




Social Plugin