Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAJALIWA ASTAAFU KUGOMBEA UBUNGE RUANGWA BAADA YA MIAKA 15 YA UTUMISHI



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la ruangwa Mkoa wa Lindi takribani miaka 15 ya uongozi wake 

Na Regina Ndumbaro Ruangwa -Lindi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ametangaza rasmi kutogombea tena ubunge wa Jimbo la Ruangwa, mkoani Lindi, baada ya kuongoza kwa takribani miaka 15 mfululizo tangu mwaka 2010.

Akiwa jimboni kwake kwa siku kadhaa za mashauriano na wananchi pamoja na wazee wa Ruangwa, Majaliwa amesema uamuzi huo umetokana na tafakari ya kina na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali. 

Amewashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoendelea kumuonyesha kwa kipindi chote cha utumishi wake.

Taarifa ya  kustaafu kwake  imekuja siku chache tu baada ya Majaliwa kutangaza bungeni, Juni 26, 2025, kuwa anapanga kugombea tena ubunge wa jimbo hilo. 

Akiwa mbele ya wabunge, alisema anaendelea kuhitaji ridhaa ya wananchi wa Ruangwa kwa kipindi kingine, huku akieleza dhamira yake ya kuendelea kulitumikia taifa kwa moyo wa uzalendo. 

Hata hivyo, kauli hiyo imebadilika rasmi, na sasa Majaliwa amethibitisha kutogombea tena nafasi hiyo ya uwakilishi.

Majaliwa ameeleza kuwa japokuwa mara nyingi amekuwa nje ya jimbo akilitumikia taifa kama Waziri Mkuu, wananchi wa Ruangwa wameendelea kumuunga mkono bila kuyumba. 

“Ninaomba kutumia nafasi hii kusema asanteni sana, na ninamuomba Mwenyezi Mungu azidi kuimarisha mshikamano uliopo kati yetu. 

Nimeamua kupisha wengine, na nina imani Ruangwa itaendelea kuwa na mwakilishi bora,” amesema.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti, huku baadhi ya wachambuzi wa siasa wakitafsiri hatua hiyo kama ya busara na ya kiungwana, hasa ikizingatiwa kuwa Majaliwa amemaliza miaka 10 kama Waziri Mkuu tangu ateuliwe mwaka 2015.

 Hatua hii pia  imekuja katika kipindi ambacho Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea na mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ambapo zoezi la kuchukua na kurudisha fomu lilianza rasmi Juni 28 na linatarajiwa kukamilika Julai 2, 2025.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com