Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAGEUZI YA KIJAMII :WASICHANA 300 WALIOACHISHWA MASOMO WAPEWA MWELEKEO MPYA



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Katika ulimwengu ambapo ndoto za wasicha wengi hukwama kutokana na changamoto za ujauzito wa utotoni, mradi wa Kijana Imara umeibuka kama mwanga mpya wa matumaini.

Kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), zaidi ya wasichana 300 nchini Tanzania wamepata fursa ya kuandika upya mustakabali wa maisha yao kwa kujengewa uwezo wa kielimu, kisaikolojia, na kiuchumi.

Mradi huu unatekelezwa na Restless Development Tanzania katika mikoa mbalimbali, huku Dodoma ikiwa kitovu cha mafanikio makubwa kupitia wilaya tano ambazo ni Dodoma Mjini, Chamwino, Kongwa, Bahi na Kondoa DC.

Wasichana hawa waliokuwa wakikabiliana na unyanyapaa na changamoto za malezi katika umri mdogo sasa wanapata nafasi ya kusimama tena kwa miguu yao na kufukuzia ndoto walizoziona zikififia.

Katika hafla ya kugawa vifaa vya ujasiriamali, Afisa Mradi wa Restless Development, Ally Saad, ameeleza dhamira ya mpango huu:

“Lengo letu ni kuwapa wasichana hawa nguvu ya kuamini kwamba maisha yao hayajafika mwisho. Tunawapa elimu, tunawajengea ujasiri, na kuwawezesha kiuchumi ili waweze kujitegemea na kuondokana na utegemezi,” amesema Saad.

Mafunzo yanayotolewa yanahusisha elimu ya afya ya uzazi, ujuzi wa maisha, ujasiriamali na elimu ya fedha.

Baada ya mafunzo, wasichana wanapatiwa vitendea kazi kama chelehani, vifaa vya saluni na mabanda ya kufugia kuku, hatua inayowapa uwezo wa kuanzisha biashara zao binafsi na kujipatia kipato cha kujitegemea.

Kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya, mradi huu unawaunganisha wasichana katika vikundi maalum vinavyowezesha kupata mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.

Aidha, kupitia CRDB Bank Foundation, wanapewa elimu ya kifedha na mtaji wa kuanzisha miradi midogo. Hatua hii inalenga kuwalinda wasichana dhidi ya kupata mimba ya pili kwa kuwajengea uhuru wa kifedha na uwezo wa kufanya maamuzi bora.

Veronica Baluwa, Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Buigiri, aliwatia moyo walionufaika kutumia ipasavyo fursa hiyo:

“Mmetunukiwa fursa ya kipekee,hakikisheni mnaitumia kwa juhudi na ubunifu ili kufikia mafanikio. Tunataka kuona ndani ya miezi sita mmekuwa mfano wa kuigwa na vijana wengine,” amesema Baluwa.

Aidha, Nekiweti Gayewi, Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Chamwino, amesisitiza umuhimu wa kuthamini msaada huo kuwa, “Vitendea kazi hivi ni mwanzo wa mabadiliko makubwa katika maisha yenu. Thamini kila kifaa na kila somo mlilojifunza kama vile mmevipata kwa gharama zenu binafsi,” amesema Gayewi.

Familia za walionufaika pia zimeonyesha furaha na matumaini makubwa. Mama Nyemo, mzazi wa mmoja wa wasichana hao, amesema:

“Fursa hii imemtoa binti yangu kwenye utegemezi uliomkwamisha kwa muda mrefu,naamini ujuzi wa saluni aliopewa utamjengea maisha mapya na kumwezesha kulea mtoto wake kwa heshima,” amesema kwa shauku.

Kwa upande wake, Mariam Dickson, mnufaika kutoka Chamwino, amezungumza kwa niaba ya wasichana wengine,“Tumepokea vifaa na elimu ya kutosha kuanzisha biashara ndogo. Tunaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuondokana na utegemezi na kuwa mfano wa mabadiliko katika jamii zetu,” alisema Mariam.

Kupitia mradi wa Kijana Imara, SDC na UNFPA wameonyesha kwamba kuwekeza kwa vijana, hususan wasichana waliopata ujauzito wa utotoni, si tu kunarejesha ndoto zilizopotea bali pia kunajenga taifa lenye nguvu kazi endelevu.

Mradi huu unatarajiwa kupanuka katika mikoa mingine, ukilenga kuwafikia wasichana wengi zaidi wanaohitaji msaada wa aina hii.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com