Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KOROSHO ZACHANUA TUNDURU:WAKULIMA WAFURAHIA VIUATILIFU BURE KUTOKA SERIKALINI


Baadhi ya wakulima wa zao la korosho tarafa ya Nakapanya Wilayani Tunduru wakipokea viuatilifu kutoka kwa Mwenyekiti wa chama cha Ushirika Mtetesi Adam Rashid 

Na Regina Ndumbaro- Tunduru

Wakulima wa zao la korosho katika Tarafa ya Nakapanya, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameeleza furaha yao juu ya mpango wa Serikali kutoa viuatilifu bure, wakisema umeongeza uzalishaji na kuinua kipato chao kwa kiasi kikubwa. 

Wameeleza kuwa hatua hiyo imewasaidia kukabiliana na gharama kubwa za pembejeo zilizokuwa kikwazo kwao kwa muda mrefu, hali iliyowafanya baadhi yao kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha korosho.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mtetesi (AMCOS), Adam Rashid, amesema kabla ya mpango huo, wengi walishindwa kumudu gharama za pembejeo kutokana na kipato duni, lakini sasa hali ni tofauti kwani uzalishaji umeongezeka maradufu. 

Ameongeza kuwa mfumo wa soko la bidhaa (TMX) umesaidia kuhakikisha wakulima wanapata bei nzuri na soko la uhakika, jambo lililorejesha matumaini kwao.

 “Awali bei zilikuwa tofauti kati ya chama na chama wakati korosho ni zilezile, jambo hilo lilikuwa linakatisha tamaa,” amesema Adam.

Mkulima Issa Makokola kutoka kijiji cha Nakapanya amesema uzalishaji umeongezeka kutoka chini ya tani 300 hadi kufikia kati ya tani 1,580 hadi 2,000 kwa mwaka, kutokana na upatikanaji wa pembejeo ikiwemo viuatilifu vinavyotolewa bure na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania. 

Amesema mpango huo umefufua ari ya kilimo kwa wananchi na kuhamasisha upanuzi wa mashamba ya korosho katika eneo hilo.

Meneja wa Chama cha Ushirika Namitili, Issa Wajika, ameipongeza Idara ya Ushirika ya Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru pamoja na Chama Kikuu cha Ushirika (TAMCU LTD ) kwa usimamizi bora wa ugawaji wa viuatilifu na minada ya mazao. 

Amesema kwa misimu minne iliyopita, upatikanaji wa salfa umeongezeka kutoka mifuko 5,000 hadi 15,528 kwa msimu wa mwaka 2025/2026, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza zaidi uzalishaji wa korosho katika Mkoa wa Ruvuma.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com