
Afisa kilimo na mifugo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi(kulia) akikabidhi chanjo kwa Afisa Mifugo wa Kata ya Mwamashele Gideon Mnyang'ali (kushoto) Julai 1,2025 katika ukumbi wa Halamashauri hiyo
Na Sumai Salum- Kishapu
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imegawa jumla ya chanjo 300,000 kwa ajili ya kuku wa kienyeji kwa maafisa mifugo wa Kata na Vijiji vyote vinavyounda Wilaya hiyo, ikiwa ni hatua madhubuti ya kuimarisha afya ya mifugo na kuinua kipato cha wananchi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya chanjo hizo Julai 1, 2025, Afisa Kilimo na Mifugo wa Wilaya hiyo, Mwita Mwijarubi amesema kuwa, zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, lenye lengo la kuboresha ustawi wa wananchi kupitia sekta ya ufugaji wa kuku wa kienyeji.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira ya dhati kwa kuwahudumia wananchi wake. Chanjo hizi tumepokea bila gharama yoyote, na wananchi wanatakiwa kupatiwa huduma ya kuchanja kuku wao bila kulipishwa chochote,” amesisitiza Mwijarubi.
Amebainisha kuwa, kwa muda mrefu, wafugaji wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya vifo vya kuku kutokana na magonjwa kama mdondo, mafua ya ndege, na mengineyo. Kupitia mpango huu, Serikali inatarajia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari hizo, hasa kwa wanawake na vijana ambao ndio kundi kubwa linalojishughulisha na ufugaji wa kuku kama chanzo cha kipato.
“Natoa agizo kwa wataalamu wote kuhakikisha kuwa wanatekeleza zoezi hili kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu. Kila mfugaji anapaswa kupatiwa huduma hii bila vikwazo wala malipo yoyote. Hatutakubali kusikia kuwa mwananchi ametozwa fedha kwa ajili ya huduma hii ya chanjo,” ameongeza.
Amewataka viongozi wa Vijiji, Mitaa na Wananchi kwa ujumla kushirikiana kikamilifu ili kufanikisha lengo la Serikali la kuhakikisha kila mfugaji ananufaika na shughuli za ufugaji kwa tija na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Afisa kilimo na mifugo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi(kulia) akikabidhi chanjo kwa Afisa Mifugo wa Kata ya Mwakipoya Hidaya Kiosi (kushoto) Julai 1,2025 katika ukumbi wa Halamashauri hiyo

Mratibu wa Chanjo ya Mifugo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga John Mchele akizungumza kwenye zoezi la ugawaji chanjo za kuku wa kienyeji kwa maafisa mifugo wa Kata na Vijiji Julai 1,2025

Afisa Kilimo na Mifugo Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga Mwita Mwijarubi akizungumza na Maafisa mifugo wa Kata na Vijiji kuhusu zoezi la ugawaji chanjo ya bure ya kuku wa kienyeji Julai 1,2015 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu











Social Plugin