Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika zoezi la usafi wilayani Masasi ambapo usafi huo ukiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Rachael Kasanda Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Katika kuhakikisha mji wa Masasi unakuwa safi na salama kwa wakazi na wageni wanaoutembelea, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Rachael Kasanda ameagiza kuwa zoezi la usafi lifanyike kila siku ya Jumamosi badala ya mara moja kila mwisho wa mwezi kama ilivyokuwa awali.
Uamuzi huo umetangazwa rasmi na unalenga kuimarisha hali ya usafi na mazingira safi katika mji huo wa kibiashara.
Zoezi la usafi liliofanyika hivi karibuni limehusisha watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa kushirikiana na wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali ya mji.
Wakazi wa Masasi wameshuhudia ushirikiano mkubwa baina ya sekta ya umma na binafsi katika kuendeleza jitihada za kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na rafiki kwa afya ya jamii.
Zoezi hilo limeonekana kama mwanzo mzuri wa mabadiliko chanya ya kimazingira katika mji huo.
Rachael Kasanda ametoa wito kwa wakazi wa Masasi kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha miji yote nchini inakuwa safi.
Ametoa msisitizo kuwa Masasi ni kitovu cha biashara kinachowavutia wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali kama vile Newala, Nachingwea, Tunduru na sehemu nyingine, hivyo ni muhimu kwa mji huo kudumisha usafi ili kuwa kivutio cha wageni na kukuza shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo wamelipongeza jukumu alilolianzisha mkuu wa wilaya, wakieleza kuwa ni hatua sahihi inayokwenda kuboresha mji kwa ujumla.
Wamesema kuwa kuanzishwa kwa ratiba ya usafi kila Jumamosi kutasaidia sana kuimarisha afya za wakazi, kuvutia watalii na wafanyabiashara, na pia kuupa mji wa Masasi taswira nzuri kwa wageni wanaoingia kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachael Kasanda akifanya usafi wa mazingira wilayani humo


Social Plugin