
Kikosi cha Stand United kimeanza kwa kuguswa vibaya katika mchezo wa kwanza wa Playoff ya kuwania nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Fountain Gate FC kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga.
Mchezo huo uliopigwa leo umeshuhudia timu ya Fountain Gate ikiibuka na ushindi muhimu ugenini, jambo linaloiweka katika nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaofanyika Julai 8, 2025 huko Singida.
Licha ya kucheza mbele ya mashabiki wao, Stand United walijikuta wakiruhusu mabao matatu ambayo yanawapa mlima mrefu wa kupanda ikiwa wanataka kurejea katika Ligi Kuu waliyowahi kushiriki miaka ya nyuma.
Bao pekee la kufutia machozi kwa Stand United limewapa matumaini japo kidogo kuelekea mchezo wa marudiano, lakini hali ya mambo inawataka kushinda kwa tofauti ya mabao mawili au zaidi wakiwa ugenini ili kufufua matumaini yao.
Social Plugin