Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAVUNA BILIONI 3.5 FOMU ZA UBUNGE NA UDIWANI , 'UTEUZI WA MWISHO JULAI 19'


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekusanya zaidi ya Shilingi bilioni 3.5 kutoka kwa wanachama walioweka nia ya kugombea nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Amos Makalla amesema idadi ya watia nia waliokichangamkia chama imevunja rekodi, hali inayoashiria kuimarika kwa hamasa ya kisiasa miongoni mwa wanachama.

“Takwimu za haraka zinaonesha waliochukua fomu za ubunge kwa upande wa Tanzania Bara ni 3,585 na Zanzibar 524, jumla ni 4,109 kwa majimbo 272. Hii inaonesha hamasa kubwa kwa wanachama wetu,” amesema Makalla.

Kwa upande wa ubunge na uwakilishi pekee, jumla ya watia nia ni 5,475. Kwa gharama ya Sh500,000 kwa kila fomu, chama kimeingiza zaidi ya Sh2.7 bilioni. Aidha, kwa ngazi ya udiwani, ambapo fomu huuzwa kwa Sh50,000, Makalla amesema wanatarajia zaidi ya wagombea 15,000, hivyo chama kinatarajia kukusanya Sh750 milioni.

Makalla amebainisha kuwa makundi mbalimbali ikiwemo wanawake, vijana, wasanii na wazee wamejitokeza kwa wingi, na hii inaonesha kuwa CCM ina hazina kubwa ya viongozi watarajiwa.

Kwa upande wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), jumla ya waliochukua fomu ni 640; Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ni 161, huku Jumuiya ya Wazazi ikiwa na watia nia 575. Walioweka nia kwa uwakilishi Zanzibar ni 503.

Katika hatua nyingine, CCM imetoa maagizo kwa kamati za siasa kuzingatia haki na usawa katika mchakato wa mchujo na uteuzi, ili kuepusha malalamiko na migongano.

Makalla amesisitiza kuwa vikao vya uchambuzi vitaanza Julai 4 kuanzia ngazi ya kata, wakati uteuzi wa mwisho kwa nafasi ya udiwani ukitarajiwa kufanyika ngazi ya mkoa kuanzia Julai 9. Kwa nafasi za ubunge na uwakilishi, uteuzi wa mwisho utafanywa na Kamati Kuu ya CCM kuanzia Julai 19, 2025.

Amewataka wajumbe wa vikao vya uteuzi kutenda haki kwa kuzingatia sifa na uwezo wa wagombea, huku akionya dhidi ya matumizi ya “orodha za mifukoni.”

“Tukatende haki, tuchague wagombea kwa misingi ya sifa na uwezo, si kwa fitina au majungu. Tunapoingia kwenye uchaguzi, tunahitaji wagombea bora watakaoiwakilisha vyema CCM,” amesema Makalla.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com