
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limewakamata watu wawili akiwemo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika, Ferdinand Antony, kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya kijana Enock Mhangwa.
Watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya video ya kusikitisha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikionesha Enock akiwa amefungwa mikono na kupigwa fimbo na watu wanaodaiwa kuwa ni viongozi wa vijiji na mgambo.
Taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa leo Julai 4, 2025, imeeleza kuwa tukio hilo lilitokea tarehe 26 Juni 2025, na lilisababisha kifo cha kijana huyo kutokana na kipigo kikali alichopokea kutoka kwa watu hao waliomshambulia huku wakiwa wamemzuia mikono.
"Jeshi la Polisi lingependa kutoa ufafanuzi wa picha mjongeo inayosambazwa mitandaoni, inayoonyesha kijana aliyefungwa mikono huku akipigwa kwa fimbo. Tukio hilo lilisababisha kifo cha Enock Mhangwa," taarifa hiyo imeeleza.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Ferdinand Antony, Mtendaji wa Kijiji cha Liyobahika, na Hussein Madebe.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine watatu ambao ni Mtendaji wa Kijiji cha Uyovu pamoja na mgambo wawili waliokimbia baada ya tukio.
Tukio hilo limeibua masikitiko makubwa katika jamii baada ya mwanaharakati Godlisten Malisa kupakia video fupi mbili kwenye ukurasa wake wa Instagram. Katika video ya kwanza, Enock anaonekana akiwa amefungwa mikono huku akibebwa na kukimbizwa na watu waliovalia kiraia katika eneo linaloonekana kuwa ni porini.
Katika video ya pili, Enock anaonekana akipigwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili huku akilia na kuomba msaada, lakini hakuna aliyekuwa tayari kumwokoa.
Social Plugin