Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Serikali imesema haitavumilia tabia ya baadhi ya wasanii kutumia majukwaa ya sanaa kama njia ya kuchochea matumizi ya dawa za kulevya, huku ikibainisha mafanikio makubwa katika operesheni za kudhibiti mihadarati kwa mwaka 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William M. Lukuvi amesema kuwa maudhui ya nyimbo, mitindo ya mavazi, na video zenye viashiria vya utumiaji wa dawa za kulevya vinakiuka maadili na sheria za nchi, hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.
Katika taarifa yake kwa Bunge kuhusu Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2024, Mhe. Lukuvi alibainisha kuwa bangi imeendelea kuongoza kwa kukamatwa zaidi, ambapo jumla ya tani 2,307.37 zilinaswa nchini. Kati ya hizo, tani 2,303.2 zilitoka mashambani ndani ya Tanzania, na tani 4.17 zilikuwa ni Skanka kutoka nchi za Kusini mwa Afrika.
"Skanka hii ni aina hatarishi ya bangi yenye kiwango cha juu cha kemikali ya THC, na idadi yake imeongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka 2023. Hili linaonyesha mafanikio ya udhibiti wa mipaka yetu," alieleza Lukuvi.
Aidha, Serikali ilifanikiwa kukamata tani 1.7 za methamphetamine, kilo 433.02 za heroin, gramu 853 za cocaine na kwa mara ya kwanza, kilo tano za dawa mpya ya MDPV (methylene-dioxy-pyrovalerone), ambayo ilikuwa ikiingizwa nchini.
Zaidi ya hayo, tani 18.45 za mirungi, kilo 56.78 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, pamoja na tani 29.6 za kemikali bashirifu zilinaswa kupitia mifumo ya ufuatiliaji wa kielektroniki.
Katika upande wa huduma kwa waathirika, vituo 16 vya methadone vilitoa tiba kwa waraibu 17,975, huku nyumba 62 za upataji nafuu (sober houses) zikihudumia waraibu 17,230 kwa mwaka huo.
Waziri Lukuvi alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kwa vitendo taasisi zinazohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya, pamoja na vyombo vya ulinzi, wataalamu wa afya na wananchi.
“Hili si janga la sekta moja, linagusa elimu, ajira, usalama na ustawi wa jamii. Ushirikiano wa wadau wote unahitajika kwa mafanikio ya kweli,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, alieleza kuwa kazi za wasanii zinaanza kugeuka chombo cha ushawishi hasi kwa vijana.
"Tunaona nyimbo na video zinazoonyesha wazi matumizi ya bangi na mavazi ya aibu yanayochochea mmomonyoko wa maadili. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria," amesema Kamishna Lyimo.
Ameongeza kuwa baadhi ya kazi hizo za sanaa zimekuwa zikisambazwa kupitia mitandao ya kijamii, na kwamba mamlaka zinafuatilia kwa karibu ili kuchukua hatua stahiki.
“Sanaa ifundishe, ijenge na ibebe maadili. Hatutakubali iwe chombo cha kupotosha kizazi,” alisisitiza kwa msisitizo mkubwa.
Serikali imehimiza jamii kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya, ili kuhakikisha Tanzania inasalia kuwa taifa salama na huru dhidi ya mihadarati.
Social Plugin