Baadhi ya wakulima wa mahindi wakisafisha mahindi hayo kabla ya kuuza kwa wakala wa Hifadhi ya Chakula( NFRA)kanda ya Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro-Ruvuma
Wakulima wa mahindi Mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kufungua soko la ununuzi wa mahindi mapema, ili waweze kunufaika na bei nzuri ya Sh.500 hadi 700 kwa kilo moja badala ya kuuza kwa wafanyabiashara wanaopita mashambani kununua kwa bei ya chini ya Sh.300 hadi 400.
Wamesema kuchelewa kufunguliwa kwa soko kunawaweka katika hatari ya hasara kubwa kwa kuwa hawana uwezo wa kuhimili gharama za kusafirisha mahindi hadi kwenye vituo vya ununuzi vilivyopo mbali.
Baadhi ya wakulima akiwemo John Nchimbi wa Matiri, Athanas Komba na Erasto Mapunda kutoka Magagura, wamesisitiza kuwa mahitaji ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya wanafunzi kurudi shule mwezi ujao ni makubwa, hivyo kuchelewa kwa soko kunaathiri maisha yao ya kila siku.
Wameipongeza Serikali kwa bei nzuri inayotolewa kupitia NFRA lakini wameomba soko lifunguliwe haraka ili wasiuze kwa madalali kwa bei duni.
Agatha Mapunda, mmoja wa wakulima, ameishauri Serikali kuruhusu wakulima wenye uwezo kuuza mahindi nje ya nchi kwa kuwa NFRA haiwezi kununua mahindi yote yanayozalishwa.
Pia ameomba kuwe na mfumo wa ununuzi unaowalenga wakulima wadogo, badala ya kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara na wakulima wakubwa pekee.
Kwa upande wake, Sebastian Komba mkazi wa Lukarasi, ameitaka NFRA kuongeza vituo vya ununuzi katika Wilaya ya Mbinga, kwani kituo pekee cha Kigonsera hakitoshelezi wakulima kutoka kata nane zenye uzalishaji mkubwa wa mahindi.
Kwa msimu wa 2024/2025, NFRA Kanda ya Songea ilivuka lengo la kununua tani 72,000 kwa kununua tani 118,292, hali iliyoonyesha hamasa kubwa miongoni mwa wakulima kutokana na bei nzuri ya ununuzi iliyoanza kwa Sh.500 na kuongezeka hadi Sh.700 kwa kilo.
Social Plugin