Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEHAMA KULETA MAGEUZI KWENYE UTUMISHI WA UMMA



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.

Akizungumza leo June 17,2025 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi rasmi wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Chinangali Park, Simbachawene amesema mifumo ya TEHAMA inayotumika sasa imesaidia kuondoa urasimu na kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma.

Amebainisha kuwa Serikali imefanikiwa kuanzisha mifumo mbalimbali ya kidijitali inayowezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa uwazi na kwa wakati, huku wananchi wakipata huduma kwa haraka na ufanisi zaidi.

Amesema maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma kuonesha ubunifu, kupokea mrejesho kutoka kwa wananchi na kubadilishana uzoefu juu ya namna bora ya kutoa huduma kwa jamii, huku akiitaka kila taasisi ya Serikali kuhakikisha inashiriki kikamilifu kutoa huduma za papo kwa papo kwa wananchi katika kipindi chote cha wiki ya utumishi.

“Kaulimbiu ya mwaka huu inatukumbusha umuhimu wa kutumia mifumo ya kidijitali kama nyenzo ya kuimarisha uwajibikaji na kuongeza uwazi serikalini. Natoa rai kwa taasisi zote kuzingatia matumizi ya TEHAMA kama sehemu ya kuleta mageuzi ya utendaji ndani ya utumishi wa umma,” amesema Simbachawene.

Aidha, amezitaka Taasisi ambazo hazikushiriki ipasavyo katika maandalizi na utekelezaji wa maadhimisho hayo kujitafakari kwa kuwa hatua hiyo ni kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Waziri huyo pia amewakaribisha wananchi wote wa Dodoma na mikoa ya jirani kutembelea maonesho hayo ya wiki nzima ili kupata huduma mbalimbali kutoka kwenye taasisi za Serikali, zikiwemo huduma za kiutumishi, elimu, afya, ardhi, biashara, umeme na nyingine nyingi.

Maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 23 Juni, yanalenga kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya nchi na Bara la Afrika kwa ujumla, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Afrika yaliyopitishwa tangu mwaka 1994.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com