Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAARIFA YA UCHUMI 2024 NA MPANGO WA MAENDELEO 2025/26 KWA MUHTASARI




Na Dotto Kwilasa, DODOMA

Serikali imetaja sekta tano zilizoongoza kwa kasi ya ukuaji mwaka 2024 kuwa ni: sanaa na burudani (17.1%), uzalishaji na umeme (14.4%), habari na mawasiliano (14.3%), fedha na bima (13.8%) na afya (10.1%).

Hata hivyo, sekta tatu zimechangia karibu nusu ya pato la taifa: kilimo (26.3%), ujenzi (12.8%) na madini (10.1%).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akiwasilisha taarifa rasmi bungeni, alisema Pato Halisi la Taifa lilifikia trilioni 156.6 mwaka 2024, likikua kwa asilimia 5.5 kutoka trilioni 148.5 mwaka 2023.

Ukuaji huo umechangiwa na uzalishaji katika Bwawa la Umeme la Julius Nyerere, miradi mikubwa ya miundombinu, mikopo kwa sekta binafsi, na uwekezaji katika huduma za jamii.

Idadi ya watu Tanzania Bara imefikia zaidi ya milioni 64, huku pato la mtu mmoja kwa mwaka likiwa Sh. milioni 3.2 (USD 1,227.4).

Deni la Taifa hadi Machi 2025 limefikia Sh. trilioni 107.7 kutoka trilioni 91.7 mwaka 2024, likitokana na mikopo ya miradi ya maendeleo.

Mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 12.4, ambapo sekta za kilimo (41%), viwanda, biashara, na mawasiliano zimefaidika zaidi.

Kwa mwaka 2025/26, serikali imetangaza bajeti ya Sh. trilioni 18.92 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ni asilimia 33.5 ya bajeti yote ya Sh. trilioni 56.4.

Mpango huo unalenga kuimarisha kilimo, miundombinu ya usafirishaji, reli ya SGR, Shirika la Ndege (ATCL), bomba la mafuta (EACOP) na TEHAMA.

Pia, serikali inalenga kushirikiana zaidi na sekta binafsi kupitia ubia (PPP) na masoko ya mitaji ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi muhimu.

Mpango huu ni daraja kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com