Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NJOLO AJITOSA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA TUNDURU KUSINI





Mohamed Njolo akikabidhiwa fomu ya kugombea nafasi ya Ubunge jimbo la Tunduru Kusini na katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tunduru Yusuf Mabema 

Na Regina Ndumbaro

Tunduru -Ruvuma 

Jumla ya wanachama wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Tunduru, mkoa wa Ruvuma, wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. 

Katibu wa CCM Wilaya ya Tunduru, Yusuf Mabema, amesema miongoni mwao, watatu wanagombea Jimbo la Tunduru Kaskazini akiwemo aliyewahi kuwa Mbunge, Eng. Ramo Makani, huku watano wakichuana kuwania Jimbo la Tunduru Kusini. 

Mabema amewataja wanachama waliogombea Tunduru Kusini kuwa ni Mohammed Njolo, Husna Kawanga, Bora Lichanda, na Mtamila Abdul.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mohammed Njolo amesema ameamua kuomba ridhaa ya CCM ili kugombea nafasi hiyo kwa dhamira ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini. 

Amesema kwa muda mrefu jimbo hilo limekosa maendeleo ya haraka kutokana na ukosefu wa uwakilishi makini katika ngazi ya maamuzi, hasa Bungeni. 

Iwapo atateuliwa na kuchaguliwa, ameahidi kutumia fedha za mfuko wa jimbo kuboresha huduma muhimu za kijamii na kusimamia vema maslahi ya wananchi kwa vitendo.

Njolo ameongeza kuwa Jimbo la Tunduru Kusini linahitaji kiongozi madhubuti, mwenye uwezo, maono na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi. 

Amesisitiza kuwa ana nia ya kushirikiana kwa karibu na wanachama wa CCM na kuwashukuru kwa ushirikiano, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazoendelea kufanya katika kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli.

Kwa upande wake, Chifu wa kabila la Wayao wilayani Tunduru, Mtalika Mkwepu, amewataka wananchi wa jimbo hilo kutumia uchaguzi huu kama fursa ya kupata kiongozi bora. 

Amesema ni muda wa kukataa viongozi wanaotafuta madaraka kwa kutoa fedha na zawadi, na badala yake kuwachagua wale wanaoguswa na matatizo ya wananchi. 

Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi wenye uzalendo na uchungu wa kweli na maendeleo ya Tunduru Kusini.


Chifu wa kabila la Wayao wilayani Tunduru Mtalika Mkwepu akiwa katika picha ya pamoja na Mohammed Njolo baada ya kuchukua fomu 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com