Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWENGE WA UHURU WAHITIMISHA MBIO TANGA

Na Hadija Bagasha - Tanga

Mwenge wa Uhuru 2025 umehitimisha mbio zake katika Mkoa wa Tanga baada ya kukimbizwa katika Wilaya ya Tanga, ambapo umekagua miradi saba, yenye thamani ya shilingi bilioni 3.3 ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya shughuli tatu mtambuka. 

Kiongozi wa mbio za Mwenge,Ismail  Ali Ussi , amesema miradi yote 7 iliyokaguliwa na Mwenge wa uhuru katika Wilaya ya Tanga ikiwemo miradi 6 ya Halmashauri ya Jiji la Tanga imekidhi vigezo. 

Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Tanga umefanya ukaguzi wa Miradi mbalimbali ya Halmashauri ya jiji la Tanga sambamba na miradi mingine. 

Miradi hiyo yenye jumla ya thamani ya shilingi Bilion 3.3, miongoni mwa miradi hiyo iliyofanyiwa ukaguzi ni pamoja na Ujenzi wa jengo la ghorofa la chini vyumba vya madarasa manne, Ujenzi wa Ofisi ya Utawala na matundu ya vyoo katika shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo kata ya Nguvumali,
Ujenzi wa Ofisi ya kata ya Tongoni,mradi wa madarasa mawili shule ya Msingi Mwakidila.

Miradi mingine ni pamoja na, mradi wa jengo la mionzi ' X-ray' katika kituo cha Afya Makorora, Ujenzi wa Barabara ya  Sahare kwa kiwango cha Lami awamu ya kwanza na ya pili, yenye Urefu wa Mita 600 pamoja na Mradi wa Ufungaji Mita za Malipo ya Kabla za Maji chini ya Mamlaka ya maji na maji Safi Jijini Tanga ' Tanga Uwasa'.

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru 2025, alisema miradi yote iliyokaguliwa  imekidhi vigezo vinavyohitajika na kuwataka wasimamizi wa Miradi hiyo kuhakikisha inafanya kazi ipasavyo na kuhudumia wananchi kama ilivyokusudiwa. 

"Niwaombe wasimamizi wa Miradi hii ,hakikisheni inafanya kazi ipasavyo ili ilete manufaa kwa Wananchi, Wananchi wetu wanataka huduma bora,hivyo ni lazima tufanye kazi ambayo Rais ametutuma , lakini hakikisheni mnawahamasisha Wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu" ,Aliongeza Ismail.

Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Balozi Dkt.Batilda Burian, Alisema Mkoa wa Tanga una fursa nyingi za kiuchumi ambapo aliwaomba wakazi wa Mkoa huo,kuchangamkia fursa hizo ikiwemo Kilimo,

"Mkoa wetu ,una fursa nyingi za kiuchumi,hivyo  niwaombe Wakazi wa Mkoa wa Tanga,mchangamkie  fursa ,tuna Kilimo cha mazao ya chakula na Biashara, ikiwemo Mkonge,Korosho,Mihogo , mahindi na matunda ya aina mbalimbali yanapatikana katika Mkoa wetu" Alisema Dkt.Batilda

kuhusu Uchaguzi Mkuu,Dkt.Burian aliwataka Vijana kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali kupitia vyama vyao vya kisiasa,

"Niwaombe Wananchi hasa Vijana,mjitokeze kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu,muwanie nafasi mbalimbali kupitia vyama vyenu vya kisiasa" Aliongeza Dkt.Burian. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com