
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi Mhe Mohamed Nyundo akiwa katika picha ya pamoja na wakulima wa mwani na mikoko baada ya kukabidhi boti na na magari aina ya Toyo wilayani humo
Na Regina Ndumbaro Kilwa-Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amekabidhi boti mbili na magari aina ya Toyo manne kwa vikundi 19 vya wakulima wa mwani na mikoko katika kata ya Somanga, mkoani Lindi.
Kijiji cha Somanga kimepokea boti moja na magari matatu kupitia Umoja wa Wakulima wa Mwani, huku kijiji cha Marendego kikipokea boti moja na gari moja kwa kikundi cha wapandaji wa mikoko.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nyundo amesisitiza kuwa hatarajii kusikia migogoro au kesi zinazohusu matumizi mabaya ya vifaa hivyo, bali anataka kusikia maendeleo na hatua chanya zilizopatikana
Ameagiza kuwe na utaratibu mzuri wa uwazi, ambapo taarifa za mapato na matumizi zitasomwa kwa wanakikundi wote ili kila mmoja awe na ufahamu wa rasilimali zinazopatikana.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amekemea tabia ya ubinafsi ndani ya vikundi na kuwataka wanachama kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinawanufaisha wote kwa pamoja badala ya kumsaidia mtu mmoja pekee.
Ameeleza kuwa vifaa hivyo ni kwa ajili ya kuinua uchumi wa kikundi na si kwa manufaa binafsi.
Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa Wakulima wa Mwani Somanga Ndugu Hafidhu Mkumbi, ameishukuru WWF kwa kusaidia juhudi zao za kiuchumi.
Amesema kuwa msaada wa boti na toyo hizo zitachochea shughuli za uzalishaji na kuongeza kipato kwa kikundi na kwa wanachama mmoja mmoja, huku wakitazamia kupanua fursa nyingine zaidi ya utegemezi wa shughuli za baharini pekee.
Social Plugin