Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Madaba Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama akiwa tayari ameshachukua fomu ya kutetea kiti chake cha ubunge katika jimbo la Madaba
Na Regina Ndumbaro
Madaba-Songea
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Madaba, Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, ameonyesha dhamira yake ya dhati ya kuendelea kulitumikia taifa kupitia jimbo hilo kwa kuchukua rasmi fomu ya kugombea tena ubunge.
Hatua hiyo imeashiria nia ya kuendeleza mafanikio ya maendeleo aliyoasisi katika awamu zilizopita, akiwa na lengo la kuinua ustawi wa wananchi wa Madaba kwa vitendo.
Mhagama ambaye amekuwa chachu ya maendeleo katika maeneo ya afya, elimu, barabara na umeme vijijini, amesisitiza kuwa dhamira yake bado ni thabiti katika kuhakikisha huduma bora kwa wananchi.
Akiwa kiongozi mwenye rekodi ya uwajibikaji na uzalendo, amesema kuwa kazi kubwa iliyoanzishwa inahitaji kukamilishwa kwa kasi na weledi zaidi.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Mhagama amewashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi cha nyuma, huku akiahidi kuendeleza uhusiano wa karibu uliopo kati yake na wananchi.
Amesisitiza kuwa endapo atapewa ridhaa tena, atahakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa uwazi, kasi na ufanisi katika kila kata ya jimbo hilo.
Social Plugin