Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rechal Kasanda akitoa vyeti kwa baadhi ya washiriki wa bonanza hilo uwanja wa sabasaba mkuti wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Zaidi ya washiriki kutoka mikoa tisa nchini wamekusanyika leo Juni 15, 2025 katika Bonanza maalum lililofanyika wilayani Masasi.
Bonanza hilo lilianzia Uwanja wa Bomani kuanzia saa 12 asubuhi, na kupitia maeneo ya Stendi Kuu pamoja na kata za Migongo, Jida na Mkuti.
Lengo kuu la bonanza hilo lilikuwa ni kuimarisha afya, kuhamasisha mshikamano wa jamii na kutoa elimu ya uchangiaji damu.
Tukio hilo liliandaliwa na Umoja wa Jogging Fitness Club Masasi chini ya viongozi wao: Haji Chimango (Katibu), Ibrahim Issa Likwembe (Mwenyekiti), na Mikidadi Likwata (Katibu wa Bonanza).
Mgeni rasmi wa Bonanza hilo ni Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Mheshimiwa Rachel Kasanda, ambaye ameshiriki mazoezi ya pamoja na baadaye kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Mji Masasi.
Katika ziara hiyo, ametembelea wodi ya watoto na kutoa zawadi kwa wagonjwa, jambo lililopokelewa kwa furaha na shukrani kutoka kwa Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Nelson Kimaro, aliyempongeza kwa kugusa maisha ya wagonjwa kwa vitendo.
Baadaye, akiwa kwenye Uwanja wa Sabasaba Mkuti, Mh. Kasanda amezungumza na wananchi na washiriki wa bonanza ambapo amewahamasisha kushiriki michezo kama njia ya kujenga afya, kuimarisha mawasiliano na kukuza undugu.
Aidha, amewaasa kujiandaa kushiriki kwa amani katika uchaguzi mkuu ujao, huku akipokea changamoto mbalimbali kutoka kwa Umoja wa Jogging Club Masasi na kuahidi kuzifanyia kazi.
Viongozi wa Jogging Fitness Club Masasi wamemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa ushiriki wake wa karibu katika tukio hilo pamoja na washiriki wote waliojitokeza.
Wamesema bonanza hilo limeonyesha mshikamano mkubwa wa kitaifa na kuahidi kuendelea kuandaa matukio kama hayo kwa ustawi wa jamii.
Social Plugin